Date: 
26-07-2024
Reading: 
Waebrania 10:19-22

Ijumaa asubuhi tarehe 26.07.2024

Waebrania 10:19-22

19 Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu,

20 njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake;

21 na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;

22 na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi.

Neema ya Kristo yatuwezesha;

Ni ujumbe wa kuishi katika Kristo kwa ukamilifu wa imani, kwa sababu waaminio wameokolewa na Kristo mwenyewe. Kristo aliyeuokoa ulimwengu ndiye Kuhani Mkuu ambaye wamwabuduo huupata ujasiri katika yeye pale wamtumaipo daima. 

Mwandishi anaonesha tumaini kwa hao waaminio pasipo kuchoka siku zote kwamba wanayo hatma njema;

Waebrania 10:37-39

37 Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.
38 Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.
39 Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.

Ujumbe tunaopewa asubuhi ya leo ni kuwa tumeokolewa na Yesu Kristo kwa neema, hivyo tuwe na ujasiri katika yeye tukijua atarudi tena kwa mara ya pili. Tukidumu katika neema hii tunakuwa na uhakika wa kuurithi uzima wa milele pale atakaporudi tena. Uwe na siku njema. Amina

Heri Buberwa