Date: 
25-07-2024
Reading: 
2 Wakorintho 1:12-14

Alhamisi asubuhi tarehe 25.07.2024

2 Wakorintho 1:12-14

12 Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi.

13 Maana hatuwaandikii ninyi neno, ila yale msomayo, au kuyakiri; nami nataraji ya kuwa mtayakiri hayo hata mwisho;

14 vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kwamba sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana wetu Yesu.

Neema ya Kristo yatuwezesha;

Mtume Paulo anawaandikia Wakorintho kuwa hawatakiwi kujisifu kwa namna yoyote ile, bali kuishi katika wokovu utokao kwa Yesu Kristo kwa neema tu. Paulo anawataka Wakorintho siyo kusoma tu na kulisikia neno la Mungu, bali kulishika hata mwisho. Mkazo wa Paulo ni kumkiri Yesu Kristo kama Mwokozi, na kwamba amewaokoa wanadamu kwa neema.

Ujumbe tunaopewa asubuhi hii ni kukumbuka wakati wote kuwa sisi tulivyo, maisha yetu na mafanikio yote tuliyo nayo, ni kwa sababu ya neema ya Mungu ambaye hutufanya tuonekane kustahili pasipo kustahili. Kwa hiyo kama Paulo anavyosema, tusijisifu kwa lofote, bali tuendelee kumkiri Yesu kwa njia ya neno lake ili tuwe na mwisho mwema. Amina

Alhamisi njema

 

Heri Buberwa