Alhamisi asubuhi tarehe 18.07.2024
2 Wakorintho 1:3-7
3 Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
4 atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.
5 Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo.
6 Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda kazi yake kwa kustahimili mateso yale yale tuteswayo na sisi.
7 Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja.
Wito wa kuwajali wengine katika Kristo;
Mtume Paulo anamtukuza Mungu atoaye faraja katika hali zote ili waaminio wapate kuwafariji wengine. Paulo anazidi kusema kuwa kwa jinsi mateso katika Kristo yanavyozidi, faraja ya waaminio pia huzidi. Faraja anayoielezea Paulo ni ile itendayo kazi kwa kustahimili mateso kwao wamwaminio Kristo.
Ujumbe wa Paulo ni kuwa waaminio hupata faraja ya Kristo na kuwafariji wengine. Kumbe tunaalikwa kuwa faraja ya wengine. Ukimpa mwenzako faraja unakuwa umemjali. Tunaalikwa kukaa pamoja katika Kristo tukishirikiana siku zote katika maisha yetu katika kuujenga mwili wa Kristo. Wajali wengine, ni agizo la Kristo. Amina.
Alhamisi njema
Heri Buberwa