Jumatano asubuhi tarehe 17.07.2024
Luka 10:30-35
30 Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.
31 Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.
32 Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.
33 Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,
34 akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.
35 Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.
Wito wa kuwajali wengine katika Kristo;
Alikuwepo mwanasheria mmoja ambaye alimuuliza Yesu kwamba afanye nini ili aurithi uzima wa milele. Yesu akamuuliza torati husemaje? Mwanasheria akaonesha kuwa anaijua torati, akajibu imeandikwa mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote, na jirani yako kama nafsi yako.
Yesu alimwambia kuwa alijibu vema, afanye hivyo naye ataishi. Sasa baada ya hapo yule mwanasheria alitaka kuonekana mwenye haki, akamuuliza Yesu kuhusu jirani, kwamba jirani yangu nani?
Ndipo tunasoma Yesu akitoa mfano wa msafiri aliyeangukia mikononi mwa wanyang'anyi, wakampiga wakimuacha karibu na kufa. Kuhani alimpita kando yule msafiri, Mlawi naye akapita kando. Ni Msamaria tu aliyemuona akamhurumia na kumpeleka nyumba ya wageni, na kugharamia matibabu yake.
Msamaria alishughulika na msafiri aliyepigwa na wanyang'anyi. Kwa mujibu wa tafakari ya juma hili, Msamaria alimjali yule ndugu katika Kristo. Ndivyo Yesu hutualika kila siku kila mmoja wetu kumjali mwenzake, yaani kukaa pamoja katika Kristo tukipendana na kushirikiana katika kazi zetu kwa Utukufu wa Mungu. Amina
Jumatano njema
Heri Buberwa