Date: 
08-05-2024
Reading: 
Matendo ya Mitume 3:1-10

Jumatano asubuhi tarehe 08.05.2024

Matendo ya Mitume 3:1-10

1 Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa.

2 Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.

3 Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.

4 Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi.

5 Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.

6 Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.

7 Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.

8 Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu.

9 Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu.

10 Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata.

Ombeni nanyi mtapata;

Mtu kiwete tangu kuzaliwa amekaa mlangoni hekaluni akiomba chochote kwa wanaoingia kusali. Aliwatazama Petro na Yohana akitarajia kupata kitu kwao, lakini ajabu Petro akamwambia sina fedha. Petro akaamuru asimame aende kwa jina la Yesu. Yule kiwete akatembea, ikawa ajabu kwa wengi.

Ipo tafsiri ya somo hili kwamba viwete wanatakiwa kuombewa tu watembee! Ni jambo jema na sahihi, Lakini hata wanaojinasibu hivyo hawajaweza kwa viwete wote! Sikatai maombi, lakini palipo uponyaji wa sala tu Roho wa Mungu huonesha. Hivyo siyo kiwete tu, ni ugonjwa wowote, na shida yoyote, lazima itatuliwe tukimtanguliza Bwana kwa kuomba tukitimiza wajibu wetu. Omba, tafuta, bisha.

Ujumbe muhimu kwa somo hili ni kuwa kiwete alipata kutembea kwa jina la Yesu. Kumbe hapa tunakumbushwa kuwa tuombe katika jina la Yesu. Amina. 

 

Heri Buberwa