Date: 
20-03-2024
Reading: 
Mathayo 20:24-28

Hii ni Kwaresma 

Jumatano asubuhi tarehe 20.03.2024

Mathayo 20:24-28

24 Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili.

25 Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.

26 Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;

27 na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu;

28 kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Kwa Yesu kuna upatanisho wa kweli;

Bwana Asifiwe;

Katika Injili tuliyosoma, ukianzia nyuma kidogo mstari wa 20, unaona mama yao wana wa Zebedayo na wanawe wakimwendea Yesu, wakimwomba hao wanafunzi wawili wakae mmoja kulia kwa Yesu, na mwingine kushoto. Injili ya Marko huwataja kama Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo wakiwa na mama yao.

Yesu aliwaambia kuwa hawajui walichokiomba, kwamba ingewezekana wao kunywea kikombe chake, hata ubatizo wake wangebatizwa, lakini habari ya kukaa kulia au kushoto kwa Yesu ni kwa ajili ya waliowekewa tayari.

Ni baada ya tukio hilo, ndipo somo letu linakuja, kwamba wanafunzi wengine kumi waliobaki waliposikia Yohana na Yakobo wanaomba kukaa na Yesu, waliwakasirikia. Yesu anawatuliza, akiwasihi kuwa wanyenyekevu (27). Yesu anasema alikuja kutumika na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. Tuwe wanyenyekevu katika kumfuata Kristo ili tuwe na mwisho mwema. Amina

Siku njema

Heri Buberwa