Date: 
13-03-2024
Reading: 
Isaya 65:17-25

Hii ni Kwaresma 

Jumatano asubuhi tarehe 13.03.2024

Isaya 65:17-25

17 Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.

18 Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.

19 Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.

20 Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.

21 Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.

22 Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.

23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na Bwana, na watoto wao pamoja nao.

24 Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.

25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng'ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana.

Furahini katika Bwana siku zote;

Ni ujumbe wa Bwana kwa Taifa lake kupitia kwa Nabii Isaya, baada ya kuwa wametoka uhamishoni. Isaya anatumia lugha ya kuumba mbingu na nchi mpya, kwa maana ya Bwana kuwakomboa na kuwarejesha watu wake toka utumwani. Ni ujumbe wa wao kufanya shangwe, na ahadi ya kustawi kwao wakidumu katika kumcha Bwana.

Ahadi ya Bwana ya Taifa lake kukaa kwenye nchi yao inatolewa katika somo hili. Kwa sasa naweza kusema ahadi ya Mungu kwetu ya kuishi maisha ya ushindi tukimtegemea Kristo ipo siku zote. Sisi tumekombolewa na Yesu kwa njia ya kifo msalabani, hivyo hatutakiwi kuwa na shaka katika, bali tufurahi katika yeye siku zote ili tuurithi uzima wa milele. Amina.

Jumatano njema 

Heri Buberwa