Date: 
22-01-2024
Reading: 
Kutoka 34:29-35

Jumatatu asubuhi tarehe 22.01.2024

Kutoka 34:29-35

29 Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye.

30 Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia.

31 Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao.

32 Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai.

33 Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake.

34 Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa.

35 Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.

Utukufu wa Mwana wa Mungu.

Musa anashuka toka mlimani akiwa tayari na maelekezo toka kwa Bwana kwenda kwa Taifa lake. Bwana alikuwa amemtokea Musa huko mlimani na uso wake uling'aa. Haruni na wana wote wa Israeli waliogopa hata kumkaribia Musa, kwa jinsi uso wake ulivyong'aa. Kwa kuuona uso wa Musa uking'aa, wana wa Israeli waliuona Utukufu wa Mungu kupitia kwa Musa, na Musa alitimiza wajibu wake kwa kuwapa maelekezo aliyopewa na Bwana.

Israeli waliuona Utukufu wa Mungu kwa uso wa Musa kung'aa. Musa alikuwa kiongozi wao kuelekea nchi ya ahadi. Historia ya ukombozi wa mwanadamu inatuleta hadi zama za Agano jipya, ambapo Yesu aling'aa mlimani akiwa na Petro, Yakobo na Yohana (Mk 9:2-8). Kung'aa kwa wote wawili kunaonesha Utukufu wa Mungu, lakini Yesu ni zaidi ya Musa kwa sababu Utukufu wake ulionekana kama Mwana wa Mungu, Mwokozi wa Ulimwengu. Mwamini sasa uokolewe. Amina.

 

Heri Buberwa Nteboya 

Mlutheri