Date: 
09-12-2023
Reading: 
Marko 1:14-15

Hii ni Advent 

Jumamosi asubuhi tarehe 09.12.2023

Marko 1:14-15

14 Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,

15 akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.

Bwana analijia Kanisa lake;

Yesu baada ya kubatizwa na Yohana, na baada ya Yohana kutiwa gerezani anaanza utume wake akiwaambia watu kutubu na kuiamini Injili maana ufalme umekaribia. Kutubu ndiyo ujumbe wa kwanza wa Yesu alipoanza huduma yake. Injili ya Mathayo hulieleza hili;

Mathayo 4:17

Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.

Leo asubuhi tunakumbushwa kuishi maisha ya toba. Sisi ni wenye dhambi, ndiyo maana huwa tunahimizwa kutubu kila wakati. Unaweza kuona kuwa tukianza ibada tunaungama, tukimaliza ibada tunaungama kwenye sala kuu tukisema "utusamehe makosa yetu". Hivyo maisha ya mkristo yanategemea toba kutoka kwa Mungu tunayemkosea ili aturehemu wakati wote. Tukitubu dhambi zetu, Yesu anatusamehe na kutupa uzima wa milele. Amina 

Jumamosi njema 

Heri Buberwa