Date: 
20-11-2023
Reading: 
2Petro 3:1-7

Jumatatu asubuhi tarehe 20.11.2023

2 Petro 3:1-7

1 Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha,

2 mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.

3 Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

4 na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

5 Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

6 kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

Hukumu ya mwisho inakuja;

Petro anaandika kuhusu hukumu ya mwisho akiliusia Kanisa kutoliacha neno la Mungu. Anahakikisha kuwepo kwa hukumu kwa watu wote, lakini akisisitiza kutomuacha Yesu katika kuingojea siku hiyo. Katika mstari wa saba Petro anasema ipo hukumu, na moto umeandaliwa kwa wote wasiomcha Mungu. Yaani wasiomcha Mungu wataangamia siku hiyo ya hukumu.

Ukiendelea kusoma unauona msisitizo wa hukumu;

2 Petro 3:9-10

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

Kumbe hukumu ipo, inakuja. Siyo lengo la Mungu tuukose uzima wa milele, bali wote tuupate. Ndiyo maana anatupa nafasi ya kufanya maandalizi. Yaani kuishi maisha ya imani, toba na msamaha ndiyo njia ya kuurithi uzima wa milele. Dumu katika yote ukitenda yakupasayo katika safari ya imani, ukikumbuka kuwa hukumu ya mwisho inakuja. Amina.

Uwe na wiki njema.

Heri Buberwa