Jumatano asubuhi tarehe 02.08.2023
2 Wakorintho 7:5-12
5 Kwa maana hata tulipokuwa tumefika Makedonia miili yetu haikupata nafuu; bali tulidhikika kote kote; nje palikuwa na vita, ndani hofu.
6 Lakini Mungu, mwenye kuwafariji wanyonge, alitufariji kwa kuja kwake Tito.
7 Wala si kwa kuja kwake tu, bali kwa zile faraja nazo alizofarijiwa kwenu, akituarifu habari ya shauku yenu, na maombolezo yenu, na bidii yenu kwa ajili yangu, hata nikazidi kufurahi.
8 Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu.
9 Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote.
10 Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.
11 Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.
12 Basi, ijapokuwa naliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu.
Wema wa Mungu watuvuta tupate kutubu;
Mtume Paulo anaelezea unyonge waliokuwa nao walipofika Makedonia akiwa na wenzake. Lakini anakiri Mungu kuwafariji. Katikati ya faraja hiyo, Paulo anaonesha kuwa watu wa Korintho waliguswa na Injili wakatubu. Na hili ndilo lilikuwa lengo la Mungu kupitia kwa Mtume Paulo, kwamba watu wake watubu.
Furaha ya Mtume Paulo ni kuwa watu wa Korintho walisikia Injili wakahuzunika kwa sababu ya dhambi zao, wakatubu. Na huu ndiyo mpango wa Mungu, kwamba wote tutubu dhambi zetu na kumtegemea yeye siku zote. Amina.
Siku njema.
Heri Buberwa