Date:
16-06-2023
Reading:
Mathayo 6:22-23
Ijumaa asubuhi tarehe 16.06.2023
Mathayo 6:22-23
22 Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.
23 Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!
Mungu au Ulimwengu;
Bwana Asifiwe;
Asubuhi hii tunalo somo ambalo ni sehemu ya hotuba ya mlimani. Katika sehemu hii Yesu anaonesha kuwa jicho likiona vizuri, basi mwili wote unakuwa na nuru. Lakini jicho likiwa bovu, basi mwili wote unakuwa giza. Nuru ikiwa ndani ya mtu hata kama jicho ni bovu, siyo giza hilo!
Fundisho hili linaandikwa pia kwenye Injili ya Luka ambapo linafafanuliwa zaidi;
Luka 11:34-36
34 Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. 35 Angalia basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. 36 Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga wake.Yesu alitoa mfano mfupi wa jicho kuona kusisitiza umuhimu wa kumjua yeye (Yesu). Tukimjua Kristo, yaani jicho likiona, tunauona utukufu wa Mungu. Tunatenda kwa jinsi tunavyoona na bila shaka tunafanikiwa. Kama jicho lako ni bovu (yaani hauko na Yesu) huwezi kuuona ufalme wa Mungu maana hauko na Yesu. Kuwa na jicho linaloona ni kumchagua Mungu aliye na hatma yetu. Kuwa na jicho bovu ni kuchagua Ulimwengu. Tumchague Mungu aliyetuahidi uzima wa milele.
Ijumaa njema.
Heri Buberwa
Mlutheri