Date: 
21-09-2022
Reading: 
Kutoka 34:21-28

Jumanne jioni tarehe 20.02.2022

Kutoka 34:21-28

[21]Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika.

[22]Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka.

[23]Mara tatu kila mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli.

[24]Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu ye yote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za BWANA Mungu wako mara tatu kila mwaka.

[25]Usisongeze damu ya sadaka yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu; wala hiyo sadaka ya sikukuu ya pasaka haitasazwa hata asubuhi.

[26]Vitu vya kwanza vya malimbuko ya nchi yako utavileta na kuvitia ndani ya nyumba ya BWANA Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

[27]BWANA akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya.

[28]Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.

Uwakili wetu kwa Mungu;

Katika Agano lake na Israeli, Mungu anawaamuru kufanya kazi kwa siku sita, na siku ya saba kupumzika. Na katika mavuno yao, Israeli wanaamriwa kumtolea Bwana pale wanapohudhuria mbele zake. Aliwataka kufanya kazi maana aliwapa ardhi na vyote viliyokuwamo. Aliwafanya mawakili wake, watunze alivyowapa na kumtolea.

Mungu ametuamuru kufanya kazi. Kutofanya kazi ni uvivu, ni dhambi. Mali tulizonazo haziwezi kuongezeka kama hatufanyi kazi. Hatuwezi kupata maendeleo bila kufanya kazi. Kumbe kufanya kazi ni agizo toka kwa Mungu. Anatuita kufanya kazi kama mawakili wake, na kumtolea kwa moyo wa shukrani.

Usiku mwema.