Jumamosi asubuhi tarehe 19.11.2022
Ezekieli 35:1-15
[1]Tena neno la BWANA likanijia, kusema,
[2]Mwanadamu, kaza uso wako juu ya mlima Seiri, ukatabiri juu yake,
[3]uuambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima Seiri, nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, nami nitakufanya kuwa ukiwa na ajabu.
[4]Miji yako nitaiharibu, nawe utakuwa ukiwa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
[5]Kwa kuwa umekuwa na uadui usiokoma, nawe umewatoa wana wa Israeli wapigwe kwa nguvu za upanga, wakati wa msiba wao, wakati wa mwisho wa uovu.
[6]Basi, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, nitakuweka tayari kwa damu, na damu itakufuatia; ikiwa hukuchukia damu, basi damu itakufuatia.
[7]Hivyo ndivyo nitakavyoufanya mlima Seiri kuwa ajabu na ukiwa; nami nitakatilia mbali nao mtu apitaye, na mtu arejeaye.
[8]Nami nitaijaza milima yake watu wake waliouawa; katika milima yako, na katika mabonde yako, na katika mifereji yako ya maji yote, wataanguka wao watakaouawa kwa upanga.
[9]Nitakufanya kuwa ukiwa wa daima, na miji yako haitakaliwa na watu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
[10]Kwa sababu umesema, Mataifa haya mawili na nchi hizi mbili zitakuwa zangu, nasi tutazimiliki, ijapokuwa BWANA alikuwako huko.
[11]Basi, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, nitatenda kwa kadiri ya hasira yako, na kwa kadiri ya wivu wako, ulioudhihirisha kwa kuwachukia; nami nitajidhihirisha kwao, nitakapokuhukumu wewe.
[12]Nawe utajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeyasikia matukano yako yote, uliyoyanena juu ya milima ya Israeli, ukisema, Wamefanyika ukiwa, wametiwa katika mikono yetu tuwale.
[13]Nanyi mmejitukuza juu yangu kwa vinywa vyenu, na kuyaongeza maneno juu yangu; nimesikia mimi.
[14]Bwana MUNGU asema hivi; Dunia yote itakapofurahi, nitakufanya kuwa ukiwa.
[15]Kama vile ulivyofurahi juu ya urithi wa nyumba ya Israeli, kwa sababu ilikuwa ukiwa, ndivyo nitakavyokutenda wewe; utakuwa ukiwa, Ee mlima Seiri, na Edomu yote, naam, yote pia; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Jiandae kwa hukumu ya mwisho;
Mungu hakufurahiswa na nchi ambayo watu wake walikosa haki. Alitamani kuiangamiza. Ni nchi ambayo watu waliacha kumtukuza Mungu wakajitukuza wenyewe, huku wateule wa Mungu wakiumia. Mungu hakuishia kuchukia, bali kuahidi kuifanya ukiwa nchi isiyo haki.
Mifumo ya jamii yetu na nchi kwa ujumla ni muhimu ikawa ya kutenda haki kwa watu wake maana Mungu hakuumba watu wake wateseke, bali wamfurahie yeye. Mifumo inayoonea watu humchukiza Mungu, na wote waumizao wengine hutenda kinyume na neno la Mungu. Wajibika kwa matendo yako maana ni kwa matendo utahukumiwa.
Siku njema.
Heri Buberwa
Mlutheri