Siku ya Jumapili 13/05/2021 ilikuwa ni baraka kubwa kwa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral kuwapokea wageni, wanawake viongozi kutoka katika Dayosisi ya Ziwa Victoria. Viongozi hao wapatao sita (6) kutoka katika mitaa, sharika, na majimbo ya Dayosisi ya Ziwa Victoria waliongozwa na Mama Askofu Elifaraja Gulle, mwenza wa Askofu Gulle wa Dayosisi ya Ziwa Victoria.
Ziara ya viongozi hao wanawake katika Usharika wa Azaniafront iliambatana na msafara wa wanawake wengine 21 ambao walishiriki ibada katika mitaa na sharika mbalimbali za Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Wakiwa ziarani Azaniafront, viongozi hao walipata fursa ya kushiriki katika ibada za Kiswahili na Kiingereza ambapo, mbali na mambo mengine, walitoa salaam zao kwa washarika wenyeji wakitumia neno kutoka katika kitabu cha Waebrania 12:1-2.
Viongozi wa Umoja wa Wanawake kutoka Dayosisi ya Ziwa Victoria wakijitambulisha mbele ya washarika wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral wakati wa Ibada ya Jumapili. Mama Askofu Elifaraja Gulle, mwenza wa Askofu Gulle wa Dayosisi ya Ziwa Victoria akitoa salaam kwa washarika wa Azaniafront kwenye Ibada ya Jumapili.
Mbali na kubadilishana uzoefu na kupeana mikakati mbalimbali, dhumuni kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kujifunza mambo ya kiroho na kiuchumi kutoka kwa Umoja wa Wanawake wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Wanawake hao viongozi walikaribishwa na Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, Mchg. Charles Mzinga ambapo alifanya nao mazungumzo mafupi na kuwapa maelezo kuhusu usharika.
Katika hatua nyingine, viongozi hao walishiriki mazungumzo ya kina pamoja na viongozi wenzao wa Umoja wa Wanawake wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, mazungumzo ambayo yalihudhuriwa na wenyeviti na waratibu wa kamati za Umoja wa Wanawake za usharika wakiongozwa na Mama Askofu Erica Malasusa, Mama Msaidizi wa Askofu Esther Lwiza, Mama Chaplain Anna Mzinga na Mama Mchungaji Mlaki.
Picha ya pamoja ya viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront mara baada ya kuwazawadia viongozi wenzao wa Dayosisi ya Ziwa Victoria vitenge vya Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Mchungaji Charles Miznga akiwa na viongozi wengine wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral kwenye picha ya pamoja na wageni, viongozi wanawake kutoka Dayosisi ya Ziwa Victroia .
Viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral wakiwa katika picha ya pamoja na wageni wao kutoka Dayosisi ya Ziwa Victroia.
Walioshiriki kuandaa ripoti hii: Jane Mhina, Paulin Paul & Cuthbert Swai.