Alhamisi asubuhi tarehe 29.09.2022
1 Wafalme 12:20-24
[20]Ikawa, Israeli wote waliposikia ya kwamba Yeroboamu amerudi, wakapeleka watu wakamwita aje mkutanoni, wakamfanya mfalme juu ya Israeli wote; wala hapakuwa na mtu aliyeshikamana na nyumba ya Daudi, ila kabila ya Yuda peke yake.
[21]Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda, pamoja na kabila ya Benyamini, watu wateule mia na themanini elfu, waliokuwa watu wa vita, ili wapigane na nyumba ya Israeli, waurudishe ufalme tena kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani.
[22]Lakini likaja neno la Mungu kwa Shemaya mtu wa Mungu, kusema,
[23]Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na jamaa yote ya Yuda na Benyamini, na watu waliosalia, ukisema,
[24]BWANA asema hivi, Msiende, wala msipigane na ndugu zenu wana wa Israeli; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakalisikiliza neno la BWANA, wakarudi, wakaenda zao, sawasawa na neno la BWANA.
Uamuzi wa busara.
Suleimani alipokufa Rehoboamu akatawala Israeli. Yeroboamu alikuwa amekimbilia Misri huko nyuma akikimbia kuuawa na Suleimani. Yeroboamu aliposikia kifo cha Suleimani akarudi. Rehoboamu alikataa ushauri wa wazee, akafuata ushauri wa vijana akiendelea kuwaumiza zaidi makabila kumi ya Israeli. Wakajitenga upande wa Kaskazini.
Tumesoma Rehoboamu akitaka kupigana kurudisha himaya ya Kaskazini iliyojitenga, maana alibaki na kabila la Yuda na Benyamini. Neno la Bwana lilimjia Rehoboamu kuwa asiende kupigana na ndugu zake. Mfalme Rehoboamu na jamaa yote ya Yuda wakatii neno hili, kila mtu akarudi nyumbani kwake.
Rehoboamu na jamaa yote ya Yuda na Benyamini walitii neno la Bwana wakaacha kwenda vitani. Tukichagua kulifuata neno la Mungu tunatenda inavyostahili. Tuchague kumsikiliza Mungu kwa njia ya neno lake.
Alhamisi njema.