Date: 
02-12-2022
Reading: 
Zaburi 45:2-7

Hii ni Advent;

Ijumaa asubuhi tarehe 02.12.2022

Zaburi 45:2-7

[2]Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; 

Neema imemiminiwa midomoni mwako, 

Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.

[3]Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, 

Utukufu ni wako na fahari ni yako.

[4]Katika fahari yako usitawi uendelee 

Kwa ajili ya kweli na upole na haki 

Na mkono wako wa kuume 

Utakufundisha mambo ya kutisha.

[5]Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; 

Imo mioyoni mwa adui za mfalme.

[6]Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, 

Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.

[7]Umeipenda haki; 

Umeichukia dhuluma. 

Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta, 

Mafuta ya furaha kuliko wenzako.

Bwana anakuja tuandae mioyo yetu;

Somo la asubuhi ya leo ni wimbo wa harusi ya kifalme ambapo mwimbaji anaitambua neema ya Mungu iliyojaa baraka. Mwimbaji anakiri kuwa kiti cha enzi cha Mungu ni cha milele na milele, na ufalme wake ni wa adili. Anaendelea kuimba kuwa Mungu amejaa haki, huichukia dhukuma. 

Mwimbaji anamalizia wimbo akiahidi kutomuacha Bwana na kumshukuru milele;

Zaburi 45:17

[17]Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu 
Katika vizazi vyote. 
Kwa hiyo mataifa watakushukuru 
Milele na milele.

Tumeona kwamba ufalme wa Mungu ni wa milele. Kwa hiyo kama tulivyoona Jumapili, Yesu alikuja, huja na atakuja tena. Katika haki yake hiyo hiyo na wema wake, anatukumbusha kuwa atarudi kulichukua Kanisa. Tunapoendelea kumshukuru na kumwabudu, tusisahau kuandaa mioyo yetu, ili akirudi tuwe na mwisho mwema.

Ijumaa njema.