Date: 
13-10-2021
Reading: 
Yohana 5:1-9

Jumatano asubuhi 13.10.2021

Yohana 5:1-9

[1]Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu.

[2]Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano.

[3]Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke.

[4]Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.]

[5]Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane.

[6]Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima?

[7]Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.

[8]Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende.

[9]Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.

 

Nguvu ya imani katika Yesu Kristo;

Yesu anamponya mtu ambaye alikuwa hawezi kwa miaka thelathini na nane. Yesu alimuona akamponya, akamuamuru ajitwike godoro na kuondoka.

Tunaona nini hapa;

-Yesu anatujua tulivyo;

Yesu ndiye aliyemuona yule ndugu na kutambua kuwa alikuwa katika hali hiyo siku nyingi.

Yohana 5:6

[6]Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima?

Uponyaji ulianzia hapo, kuwa Yesu ndiye alimuona. Sasa basi, fahamu ya kuwa Yesu anatuona yote tunayofanya, anafahamu tulivyo. Hivyo kufanya uovu tukajidanganya ni bure, maana wanadamu wenzetu hawatuoni lakini Yesu anatuona. Anakuona ukiiba, ukizini, ukidanganya, ukionea wengine, ukisengenya n.k Na ukweli ni kuwa hafurahishwi na tabia hizi zilizo kinyume cha mapenzi yake. Tutubu.

-Yesu ni mwenye huruma.

Huruma yake ilimfanya amponye yule ndugu. Hakumpa masharti yoyote, kama ilivyo kwa baadhi yetu siku hizi, ambao bila kutoa sadaka hawakuombei!!!

Yesu anayo huruma, anatuita kuja kwake, akitukumbusha pia kuwa na huruma kama yeye.

-Tumia fursa vizuri 

Yule mgonjwa alitumia fursa alipokutana na Yesu. Alipoulizwa kama anataka kupona, kwa imani alijibu haraka;

Yohana 5:7

[7]Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.

Unaweza kufikiri kuwa alitaka Yesu amtie birikani, kwa maana hiyo alitaka kupona.

Hivyo alitumia fursa ya kukutana na Yesu, kupona.

Huyu ndugu anawakilisha watu wasio wavivu. Tunatumiaje fursa zinazotuzunguka kujipatia maendeleo? Au tunaishia kulalamika? Wito wangu kwako ni kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa maana kazi ndiyo msingi wa maendeleo. Yesu yuko tayari kukutia birikani, jitokeze.

Dumu katika imani ya kweli katika Yesu Kristo, maana pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu.