Date: 
03-10-2022
Reading: 
Waamuzi 13:8-14

Jumatatu asubuhi tarehe 03.10.2022

Waamuzi 13:8-14

[8]Ndipo huyo Manoa akamwomba BWANA, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa.

[9]Mungu akasikiza sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye.

[10]Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijilia siku ile.

[11]Basi Manoa akainuka, akamwandama mkewe, na kumfikilia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Naam, ni mimi.

[12]Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini?

[13]Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari.

[14]Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze.

Tuwajali watoto wetu;

Wana wa Israeli walitenda mabaya mbele za Mungu, Mungu akawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini. Baadaye Mungu alituma ujumbe kwa mke wa Manoa kwamba angemzaa mtoto wa kiume (Samsoni) ambaye angekuja kuwaokoa Israeli toka mikononi mwa Wafilisti. Somo la leo asubuhi Mungu anatuma ujumbe ule ule kwa mara ya pili, kwamba Manoa na mke wake watazaa mtoto wa kiume, wanapewa masharti. 

Mtoto aliyekuwa anatabiriwa kuzaliwa ni Samsoni aliyekuwa awakomboe Israeli. Wakati wa kumsubiria mtoto huyo, tumeona mama mtarajiwa akipewa masharti ya kuishi na kula. Alipewa masharti ili kumlinda mtoto ajaye. Naweza kutafsiri masharti yale kama njia ya kumjali mtoto ajaye. Kumbe watoto wanahitaji uangalizi toka hatua ya awali, kuzaliwa, malezi hadi wanapokua na kuwa watu wazima.

Nakutakia wiki njema yenye kuwajali watoto. Amina.