Date: 
20-01-2026
Reading: 
Mwanzo 47:1-6

Hii ni Epifania 

Jumanne asubuhi tarehe 20.01.2026

Mwanzo 47:1-6

1 Ndipo Yusufu akaja akamwarifu Farao, akasema, Baba yangu, na ndugu zangu, na kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo, wamekuja kutoka nchi ya Kanaani, nao wako katika nchi ya Gosheni.

2 Akatwaa watu watano miongoni mwa nduguze, akawasimamisha mbele ya Farao.

3 Farao akawauliza hao nduguze, Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Watumwa wako tu wachunga wanyama, sisi, na baba zetu.

4 Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya Kanaani. Basi, twakusihi, uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya Gosheni.

5 Farao akamwambia Yusufu, akisema, Baba yako na ndugu zako wamekujia;

6 nchi ya Misri iko mbele yako, palipo pema pa nchi uwakalishe baba yako na ndugu zako; na wakae katika nchi ya Gosheni. Tena ukijua ya kuwa wako watu hodari miongoni mwao, uwaweke wawe wakuu wa wanyama wangu.

Nyumba zetu hubarikiwa na Mungu;

Baada ya Yusufu kuwa ameuzwa Misri, na baada ya njaa kubwa kutokea, watoto wa Yakobo walifuata chakula huko Misri. Yusufu aliwaambia wamlete mdogo wao (Benjamin) na baadaye baba yao, hivyo familia ya Yakobo ikasafiri kutoka Kanaani kuelekea Misri. Somo la asubuhi ya leo ni Yakobo akiingia Misri yeye na familia yake. Yusufu anawahudhurisha ndugu zake mbele ya Farao, akawapa nchi ya Gosheni.

Yakobo na wanae wakaanza kukaa Misri, penye chakula tele. Mungu alimtumia Yusufu kuwanusuru na njaa. Walikuwa hawana njia nyingine zaidi ya kumtii Yusufu wakasafiri na baba yao hadi Misri ili wasife njaa. Pamoja na kumuuza Yusufu, bado Bwana hakuwaacha, wakanusurika kufa njaa. Nasi tunaye Yesu ambaye hatuachi daima. Basi tumshike yeye ambaye hubariki nyumba zetu. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa