Hii ni Epifania
Jumamosi asubuhi tarehe 17.01.2026
Matendo ya Mitume 19:1-7
1 Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;
2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.
3 Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.
5 Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.
7 Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.
Ubatizo wetu;
Paulo yuko Efeso anakutana na wanafunzi kadha wa kadha, anawauliza kama walipokea Roho Mtakatifu walipoamini. Nao wanakuwa waaminifu, wakisema siyo tu kumpokea huyo Roho Mtakatifu, hata kusikia habari zake bado! Paulo anawauliza walibatizwa kwa ubatizo upi? Wanajibu ule wa Yohana. Basi Paulo anawaambia kwamba Yohana alibatiza ubatizo wa toba, sasa wabatizwe kwa jina la Yesu. Waliposikia wakaamini, wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Naye Paulo akawawekea mikono, wakajazwa Roho Mtakatifu, wakanena kwa lugha na kutabiri.
Tunachokiona leo asubuhi ni waliokuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana, kuamini na kubatizwa kwa jina la Yesu. Paulo anatufundisha na kutukumbusha kwamba ubatizo unatoka kwa Yesu mwenyewe. Katika somo, ni baada ya kubatizwa katika jina la Bwana Yesu wanafunzi wale walimpokea Roho Mtakatifu. Kumbe tukibatizwa tunampokea Yesu Kristo, ambaye ahadi yake ni kututunza hata milele yote. Ubatizo ni wokovu kamili. Wewe mbatizwa umeokolewa, usiiache imani hii. Ubarikiwe. Amina
Jumamosi njema
Heri Buberwa
