Date: 
10-01-2026
Reading: 
Matendo ya mitume 11:19-26

Hii ni Epifania 

Jumamosi asubuhi tarehe 10.01.2026

Matendo ya Mitume 11:19-26

19 Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao.

20 Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu.

21 Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana.

22 Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia.

23 Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo.

24 Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana.

25 Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli;

26 hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.

Yesu ni nuru ya Ulimwengu;

Kanisa la Antiokia wakati wa Mitume lilikuwa na waamini wengi waliotawanyika kwa sababu ya dhiki iliyokuwa imesababishwa na habari ya Stefano. Lakini pia watu wa Kipro na Kirene waliingia Antiokia, idadi ya waaminio ikawa kubwa. Habari zikafika masikioni mwa Kanisa la Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende huko Antiokia. Alipofika alifurahi kuona neema ya Mungu juu ya Kanisa la Antiokia.

Ukiendelea kuanzia mstari wa 27 unaona watu wa Kanisa la Yerusalemu wakishuka Antiokia. Mmoja kati yao akafunuliwa kuwa kungekuwa na njaa katika dunia nzima, na kweli ilitokea siku za Klaudio. Basi wale Mitume wakaazimia kupeleka msaada kwa ndugu wote ili wasife njaa

Somo linatuonesha watu waliotawanyika kwa sababu ya kuuawa kwa Stefano. Walikata tamaa, lakini Yesu Kristo bado alikuwa nao. Hata ilipokuja njaa, bado Yesu alikuwa nao. Yaani katika shida (giza) zote, Yesu aliendelea kuwa msaada (nuru) kwao. Yesu yuko nasi hata sasa akituangazia njia zetu. Tusimuache daima. Amina

Jumamosi njema

 

Heri Buberwa 

Mlutheri