Date: 
06-01-2026
Reading: 
Isaya 49:6-12

Jumanne tarehe 06.01.2026;

Siku ya ufunuo (Epifania)

Masomo;

Zab 26:5-8

Mt 2:7-12

*Isa 49:6-12

Isaya 49:6-12

6 naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

7 Bwana, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya Bwana aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua

8 Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa;

9 kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho.

10 Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.

11 Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote.

12 Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu.

Yesu ni nuru ya Ulimwengu;

Utangulizi;

Taifa la Mungu lilikuwa limepigwa, limetekwa, hekalu limeharibiwa. Walikuwa wamepelekwa Babeli, wakitolewa kwenye nchi yao, na Mungu wao. Uhamisho huu ulikuwa mgogoro wa utambulisho wao na Imani. Kwa kuangalia tu unaweza kujiuliza; walikuwa bado watu wa Mungu? Wangemwabudu vipi ugenini? Katika mgogoro huu, Isaya analeta neno la matumaini, kwamba Mungu ataleta mtumishi wake atakayeleta haki. Kweli, inatokea katika sehemu ya pili (sura ya 40 hadi 55) ya Isaya, anaeleza kurudi kwa Israeli kwenye nchi yao, ahadi ya kulijenga upya hekalu na Taifa lao kwa ujumla. Uhamisho wa zamani unachukuliwa na maisha mapya baada ya kurudi nyumbani.

(Soma Isaya 49:1-6)

Inaonekana Isaya anatoa ujumbe wake kwa nguvu, na kwa maoni yangu kama ingekuwa ni chapisho kwa siku hizi, mstari wa 1 hadi wa 3 ingekuwa yote kwa herufi kubwa. Sababu; ujumbe siyo kwa Israeli tu, bali kwa ulimwengu wote "enyi kabila za watu mlio mbali" (mst 1). Sababu pia, ujumbe huu unatoka kwa Mungu, kwamba Mungu amemwinua mtumishi wake kwa ajili ya utukufu wake (mst 3) Kutoka kwa Rahabu hadi kwa Daudi, hadi kwa Maria, habari ya watu wa Mungu iko na watumishi wasioeleweka waliotumwa na Mungu. Haya ndiyo maudhui katika somo tunalojaribu kupitia hapa. Yupo mtumishi anayeitwa akiwa bado tumboni, amefichwa na haonekani. Mungu anamficha mtumishi "kwenye kivuli cha mkono wake" (mst 2). Hapa hata mtumishi mwenyewe haelewi kama ni mtumishi wa Mungu. Mtumishi mwenyewe pia ni kama haamini, anaishia kutubu (mst 4)

Somo lenyewe;

Ukiendelea kusoma mstari wa 7, Mungu anaona hali ya mtumishi wake, lakini anamtia moyo kuwa atatambulika na mfalme kwa sababu Mungu Mtakatifu wa Israeli amemchagua. Kwa mhubiri awaye yote, hii ni fursa ya kuona jinsi ambavyo Mungu huwaita watumishi wake, na labda zaidi, jinsi ambavyo wengine huitwa lakini bado huwa hawajitambui. Mungu ana uelekeo wa kukomboa kabila za Yakobo (mst 6). Miaka ya kuwa uhamishoni ilisababisha waishio nje (leo tungesema diaspora) kuanzia Mesopotamia (leo ni uwanda wa Iraki, Kuwait, Uturuki na Syria) hadi Misri, wakijaribu kujikwamua kimaisha. Lakini lengo la Mungu lilikuwa kuwakomboa (6) kwamba Israeli wamrudie (5). Mungu alikusudia Israeli wamrudie, kwa sababu uhamisho wao haukuwa mwisho wao. Mstari wa 9 hadi 12 ni hakikisho la kutolewa utumwani.

Ujumbe tunaoupata hapa ni kuwa "watu wa Mungu hawaishi wala kuwa peke yao, na ukombozi siyo mwisho, bali hatma yao yote iko mikononi mwake". Mungu huwakusanya watu wake kwa lengo moja; wokovu kwa ulimwengu wote. Mungu anawataka Israeli, watumishi wake kuwa nuru ya kwa mataifa, ili wokovu uwafikie watu wote.

Tuendelee;

Tumeona ambavyo Mungu alivyolipenda Taifa lake, Isaya akisimulia walivyokombolewa toka utumwani. Huu mpango ulikuwa endelevu. Na kwa mpango huu kuwa endelevu, Isaya alitabiri kuja kwa Yesu kama nuru ya ulimwengu;

Isaya 9:2
Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.

Isaya anakazia juu ya nuru hii, Yesu Kristo;

Isaya 60:19-20

19 Jua halitakuwa nuru yako tena wakati wa mchana, Wala mwezi hautakupa nuru kwa mwangaza wake; Bali Bwana atakuwa nuru ya milele kwako, Na Mungu wako atakuwa utukufu wako.
20 Jua lako halitashuka tena, Wala mwezi wako hautajitenga; Kwa kuwa Bwana mwenyewe atakuwa nuru yako ya milele; Na siku za kuomboleza kwako zitakoma.

Baada ya Yesu kuja, alijitambulisha kama nuru ya ulimwengu;

Yohana 8:12

Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.

Yesu anajitambulisha kama nuru. Nuru huangaza gizani. Alikuja kututoa gizani (dhambini) hivyo tunawajibika kumwamini kama alivyosema;

Yohana 12:46

Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.

Tukimwamini Yesu tunatoka gizani. Epifania ya mwaka huu nakuomba utafakari, uko gizani au nuruni?

Epifania njema.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com