Hii ni Noeli;
Jumanne asubuhi tarehe 30.12.2025
Zaburi 109:21-26
21 Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako, Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe.
22 Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji, Na moyo wangu umejeruhi ndani yangu.
23 Ninapita kama kivuli kianzacho kutoweka, Ninapeperushwa kama nzige.
24 Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga, Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta.
25 Nami nalikuwa laumu kwao, Wanionapo hutikisa vichwa vyao.
26 Ee Bwana, Mungu wangu, unisaidie, Uniokoe sawasawa na fadhili zako.
Mungu anatimiza ahadi zake;
Baadhi ya Zaburi huwa zinaombea hukumu, msiba, bahati mbaya au laana kwa adui wa Israeli, kwa sababu pia adui hao wanatambulika kama adui wa Mungu. Zaburi ya 109 ni mojawapo ya Zaburi hizi zenye utata, zinazomuita Mungu kufanya kisasi kwa waovu wanaowasumbua watu wa Mungu. Zaburi hizi zinamuita Bwana kuwa kinyume na hawa waovu.
Daudi ni mwimbaji wa Zaburi anayeomba msaada wa Bwana (mst 26). Anataja uovu unaofanywa na adui zake, na anaomboleza juu ya mateso ya uovu huo. Maombi kwa adui zake yalikuwa makali sana na mengi, hadi ikabidi Daudi kumrudia Bwana kwa msaada na ukombozi. Daudi alikiri udhaifu wake katika kukabiliana na adui zake, akiomba msaada wa Bwana.
Sio kwamba alikuwa kwenye hatari tu ya kimwili, lakini kejeli zilizidi kumshinda kuhimili, hivyo kumrudia Bwana na kumpa moyo wake, akiomba Bwana kulipa kisasi. Daudi anatubu kwa kutokuwa na uwezo wa kuhimili watesi wake na kumlilia Mungu. Mwanzoni mwa Zaburi hii, Daudi anaorodhesha mabaya aliyofanyiwa, akiomba kisasi, lakini alivyoendelea kutaja uovu wao, akakumbuka kuwa alimtumikia Mungu aliyejaa neema na upendo, aliyeahidi kuwalinda wote wateswao kwa jina lake.
Kuna waaofikiria (na kufanya) kuwa wakristo wanatakiwa kutumia sala (maombi) "bila kujali" kuelekea kwa adui zao wakimuomba Mungu haki na udhihirisho, huku wakiombea adui zao kisasi. Wakati huohuo, katika Kanisa moja la Kristo, wapo wanaofikiri kwamba kuombea hukumu adui zao sio sahihi, kwa sababu tumeitwa kuwapenda adui zetu, na kuwaombea wanaotuudhi.
Sala za kuombea vibaya adui sio za kuchukulia kwa urahisi, labda njia ya kulielezea hili katika maisha yetu ni kuweka usawa kiBiblia, kati ya kuomba msamaha na wokovu kwa adui zetu, na kuomba haki ya Mungu itendeke.
Katika maisha ya kawaida, kuna wakati wa kupenda, kuna wakati wa kuchukia, kuna wakati wa vita, kuna wakati wa amani n.k hivyo hivyo tufahamu kuwa upo wakati wa kumwomba Mungu atuepushe na mabaya yanayotusibu, lakini siku zote tunaposali sala kuelekea adui zetu, tuombe busara ya kiMungu, atuongoze kwa Utukufu wake.
Tunapomaliza mwaka huu, ni wazi kuwa kuna sehemu tumekumbana na magumu. Sio wakati wa kutafuta adui yetu nani! Tumshukuru Mungu kwa kuwa ametuvusha salama, na ameendelea kutupa neema yake hadi tumefikia leo. Ni wajibu wetu kuwasamehe wote waliotukosea. Kusamehe ni agizo. Jihoji;
Imekuwaje wewe unaomba msamaha kwa Bwana kila siku, lakini wewe hutaki kusamehe?
Wewe mbona Bwana anakusamehe?
Unakataaje kumsamehe unayemuona? Wakati anayekusamehe humuoni? Kama ni kwa Imani kwa nini kwa Imani hiyo hiyo usimsamehe mwenzio?
Unajua kuwa usiposamehe husamehewi?
Mathayo 6:14-15
[14]Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. [15]Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.Tatizo ni pale Agano la kale, linaposomwa na kutafsiriwa moja kwa moja bila kurejea Agano jipya. Yesu alifundisha kutolipiza kisasi, pale aliposema;
Mathayo 5:38-42
[38]Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; [39]Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. [40]Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. [41]Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. [42]Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.Anaposema kwamba "mmesikia kwamba imenenwa...." anamaanisha Agano la kale. Yesu anakuja kuitimiliza torati.
Hivyo, tunapomshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka, tuwasamehe wote waliotukosea, na sisi tuombe msamaha kwa tuliowakosea, na hivi tutakuwa Taifa la Mungu, yaani watu tulio Kanisa la Mungu mwenyewe. Amina
Nakutakia sherehe njema za mwisho wa mwaka.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
Butainamwa, Bukoba
