Hii ni Noeli
Jumamosi asubuhi tarehe 27.12.2025
1 Petro 4:12-19
[12]Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
[13]Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
[14]Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.
[15]Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.
[16]Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.
[17]Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii injili ya Mungu utakuwaje?
[18]Na mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi?
[19]Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu.
Uwe shahidi mwaminifu wa Yesu;
Theologia ya kisasa inaamini mateso hayatabiriki na hayaepukiki. Kuwa hakuna tuwezalo kufanya, juu ya mateso. Tunaweza kukubali tu na kupitia mateso, na tukiishi matesho yanaisha. Mateso ni kama sumu, yaani uchafu tu, ukisafisha maisha.
Baadhi ya wachambuzi, na wakristo wengi wanaikataa Theologia hii. Kwanza kwa hoja kuwa Mungu "hasababishi" mateso, "anayaruhusu". Hakuna mateso yanayotujia, lakini yale tu Mungu ameruhusu kwa Utukufu wake. Mungu anaweza asisababishe mambo yote, lakini anasababisha mambo yote kwa uzuri, kwa wampendao na walioitwa kwa jina lake.
Warumi 8:28
[28]Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.Hivyo, waamini wengi hudhubutu kutoyaona mateso kama uzoefu hasi, lakini kama kitu chanya. Tumesoma maneno ya mwisho ya Petro kuhusu mateso ya waaminio. Petro anatoa mwelekeo wa mateso. Anaelekeza tufanye nini wakati wa mateso. Ujumbe wa Petro unalenga kujaribu kugeuza mitazamo yetu na matendo wakati wa mateso. Petro haongelei aina tofauti za mateso katika somo la leo, anaongelea tu mateso ya mkristo kwa maisha ya kila siku.
-Tunatakiwa kujua kuwa tunavyoishi, tunashiriki mateso ya Kristo. Wakati wa kazi na maisha yake hapa duniani, Yesu alipitia njia ya mateso. Kazi yake haikuwa rahisi. Alifanya kazi muda wote, akitembea kote kuwafikia wote. Lakini bado kuna waliomkataa, hawakumwamini, wakaishia kumsulibisha, na kumtesa hadi kufa. Hivyo, kwa njia ya Imani, tunashiriki mateso kwa njia ya Yesu Kristo.
-Kwa njia ya mateso, Utukufu wa Mungu unadhihirika. Mateso sio Jambo au tukio la kudumu. Tukimtegemea Mungu anatupitisha katika mateso. Na tukishashinda na kuyavuka mateso, tunamtangaza Kristo aliyeshinda, hivyo Utukufu wa Mungu kudhihirika kwa wanadamu.
-Tunapopitia mateso, tujue kuwa Yesu yupo nasi wakati wote. Tunapopata mateso, ni lazima tupite na tushinde, maana Yesu haruhusu tupate mateso yanayotuzidi. Hatuna haja kuogopa kwa sababu moja tu, kwamba; "Wanaokutesa wewe, wanakuwa wanapambana na Yesu aliyeko ndani yako"
-Petro anakazia na kueleza kuwa hukumu ipo inatusubiri. Petro anauliza; kama hukumu ipo kwa waaminio, kwa wasioamini itakuwaje? Kuepuka hukumu ni kuishi kwa kutenda yaliyo mapenzi ya Mungu, kwa kulisoma na kulitii neno lake. Tunapopitia wakati mgumu, tusikate tamaa hadi kumkosea Mungu tukaamguka, yaani tuvumilie mateso kwa ajili ya Yesu ili tuiepuke hukumu ya mwisho.
Jana tuliwakumbuka mashahidi wafia dini, watu waliokuwa tayari, na waliokufa sababu ya Imani yao. Walipitia mateso, lakini ilipolazimu, ilibidi kufa wakimtetea Kristo. Wewe unaweza?
Tunaitwa kujiweka kwa Mungu, na kumtegemea tukiitetea Imani. Tusiishi kwa kuangalia wengine wanatuonaje, bali Kristo anatuonaje. Katika kuitetea Imani, lazima Yesu tunayemtetea aonekane kwetu. Uvumilivu katika maisha yetu ni muhimu sana, tamaa itatuzuia kuiendea mbingu.
Tujiweke kwa Mungu.
1 Petro 4:19
[19]Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu.Unaitetea Imani yako?
Heri Buberwa Nteboya
Butainamwa, Bukoba
KKKT/DKMG
