Hii ni Noeli;
Alhamisi ya tarehe 25.12.2025
Siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu;
Sikukuu ya Krismasi;
Masomo;
Zab 116:1-5
Luka 2:15-20
*Isaya 9:6-7
Isaya 9:6-7
6 Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.
7 Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.
Imanueli: Mungu yu pamoja nasi;
Ujumbe wa Nabii Isaya katika siku za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu kama leo, hutumika tangu kale kwa kuwa huangazia mwanga kung'aa gizani (mst 2) na ujumbe mahususi wa mtoto aliyezaliwa kwetu kama Isaya alivyotabiri. Lakini pia ujumbe wa Nabii Isaya hupendwa zaidi kwa sababu huonesha uhakika wa ukombozi kwa wanadamu. Sababu ni kwamba Isaya alimtabiri Yesu Mwokozi ambaye angekuja kuleta furaha kwa watu wote na ukombozi kwa Taifa lake lote. Naweza kusema pasipo na shaka kwamba ujumbe kutoka kwa Nabii Isaya hupendwa kwa sababu ni unabii uliotimia. Kumbe leo tunarejea unabii kamili ambao ulitimia kwa Yesu kuzaliwa. Kwa muktadha huo, mistari inayotangulia kabla ya somo inaonesha Yesu alivyoleta nuru palipokuwa giza, na furaha kwa wote. Soma hapa chini;
Isaya 9:2-4
2 Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. 3 Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. 4 Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani.Somo lenyewe;
Isaya anaendelea kutabiri Yesu atakayezaliwa kama mtoto mwanamume ambaye uweza wa kifalme utakuwa begani mwake. Isaya anataja anaandika kwamba ataitwa;
-Mshauri wa ajabu
-Mungu mwenye nguvu
-Baba wa milele
-Mfalme wa amani
Isaya anaendelea kueleza kwamba enzi yake haitakuwa na mwisho (ndiyo maana hata sasa tunamwabudu). Isaya anatabiri Yesu kuuthibisha na kuutegemeza ufalme kwa hukumu na kwa haki.
Tangu kabla ya somo hili tulilosoma, mkazo wa Isaya ni wokovu na imani katika Bwana. Ukirudi nyuma kidogo (sura ya saba) inakadiriwa kuwa mwaka 734 - 732KK Yuda ilipokuwa inavamiwa na Israeli na Siria, Ahazi mfalme wa Yuda alipanga kutafuta msaada kutokwa kwa waAshuru. Isaya alimwambia Ahazi kusimama katika imani na kukataa ushirika wowote (7:3-9) na kumtegemea Bwana ambaye angewakomboa milele. Isaya analithibitisha hili kwa maneno ambayo yananukuliwa katika Injili ya Mathayo. Angalia;
Isaya 7:14
Kwai hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.Mathayo 1:23
Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.Kwa hiyo baada ya kuongea na Ahazi kuhusu ushindi kwa njia ya imani, anakuja kwenye sura ya tisa kumtabiri mfalme na mtawala wa haki ajaye. Sura ya tisa inakazia kwamba mfalme atakayekuja siyo wa muda tu, bali ni wa milele. Kwenye sura ya saba Isaya anamuelekeza Ahazi kwamba hata wakivamiwa wamtegemee Bwana watashinda. Anagusia ujio wa Yesu. Sasa kwenye sura ya tisa tuliyosoma ni mkazo kwamba atakuja Yesu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu.
Imanueli: Mungu yu pamoja nasi;
Neno tulilopewa kama wazo nimelinukuu kwenye tafakari ya leo (soma tena) kuonesha kwamba alitabiri Isaya, halafu imenukuliwa na Mathayo (Isaya 7:14, Mathayo 1:23). Isaya alikuwa anaonesha kwamba Yesu angekuja kwa ajili ya wanadamu. Malaika alipomtokea Mariamu alimwambia hivyohivyo akikazia ujumbe wa Isaya, kwamba Yesu yuko nasi. Tusiadhimishe siku hii kwa historia tu, bali historia itukumbushe kwamba Yesu Kristo alizaliwa kwa ajili yetu, hivyo tumpe maisha yetu ili atuokoe, atutunze na kutuongoza hadi uzima wa milele. Amina
Tunakutakia sherehe njema za Krismasi
Ni sisi;
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
bernardina.nyamichwo@gmail.com
Butainamwa, Bukoba
