Date: 
24-12-2025
Reading: 
Yohana 1:14

Hii ni Noeli;

Jumatano ya tarehe 24.12.2025;

Usiku Mtakatifu;

Masomo;

Zaburi 136:23-26; 1Yohana 1:1-4

*Yohana 1:14

Yohana 1:14

[14]Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.

Neno alifanyika mwili kwa ajili yetu;

Imani yetu imekuwa na mjadala siku zote kwa wasioifuata, kuhusu Utatu Mtakatifu. Wasioamini katika Utatu Mtakatifu wanahoji uungu wa Yesu, Mungu anayezaa, na Mungu aliyebebwa mimba. Lakini anabaki kuwa Mungu kwa kuwa kazi zake zimekuwepo, zipo na zitakuwepo zikionekana usoni pa wamtafutao. Yesu aliye neno ni Mungu aliyekuja kama mwanadamu, mwenye utukufu kutoka kwa Baba, aliyejaa neema na kweli. Mstari tuliosoma ni mwendelezo wa mwanzo wa Injili ya Yohana;

Yohana 1:1-5

[1]Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
[2]Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
[3]Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
[4]Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.
[5]Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.

Yohana anatumia "Neno" kumtaja Yesu katika Injili hii. Neno aliyekuwepo, Neno aliyekuwa Mungu, Neno aliyeumba vyote, alifanyika mwili akakaa kwetu, ni Yesu Kristo mwana wa Mungu aishiye.

"...ni ajabu kubwa katika maandiko, yanavyostaajabisha, hata kuliko ufufuo, na kustaajabisha zaidi kuliko uumbaji. Ukweli kuwa mtu, mwana wa Mungu alikuwa mwanadamu na kuwa mtu kabisa, ili Mungu aliyepo daima awe mtu mmoja na mwanadamu aliyezaliwa, kwa milele, ni ajabu kubwa sana katika ulimwengu huu..." Wayne Gruden (Systematic Theology) pg 563

Hivyo, huyu Neno anayeongelewa leo ni Yesu Kristo, ambaye alikuwepo, yupo, na atarudi kulichukua Kanisa. Muhimu kujua kuwa;

-Yesu ni Mungu

-Baba ni Mungu

-Mwana sio Baba, alikuwa na Baba

-Yesu hakuumbwa, ni wa milele.

-Yesu alitujia kama mwanadamu bila kuacha uungu wake.

Neno alifanyika mwili.

Hapa ni Yesu alipokuja duniani kama mwanadamu kuleta habari za ufalme wa Mungu. Alikuja kuhubiri na kufundisha yapasayo. Kama Neno, Yesu huyu ni Mungu kamili;

Yohana 10:30

[30]Mimi na Baba tu umoja.

Huyu Neno alipofanyika mwili, akawa mwanadamu kamili. Yesu ndiye Neno aliyekaa kwetu, na Utukufu wake ukaonekana.

Ujumbe wangu kwako;

1.Yohana anatumia picha ya "Neno" kuonyesha uungu wa Yesu na uwezo wake.

Yesu ndiye Neno aliyekuwepo toka enzi na ataendelea kuwepo.

Tunakumbushwa kuwa alizaliwa kwa ajili yetu.

2.Huyu Neno alikaa kwetu.

Hapa tunakumbushwa kuwa Yesu alikuja kwa ajili yetu sisi. 

Ilikuwa ni kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, ndio maana alikaa kwa mwanadamu.

Ni swali wewe kujiuliza; 

Amekaa kwako?

Nini kimemzuia kukaa kwako?

3.Amejaa utukufu na neema.

Yesu huyu aliyezaliwa ni mwenye utukufu.

Hapa kuna ukuu wa Mungu.

Utukufu wa Yesu hauna "ubia"

Tumpe utukufu wake sio kwa kuongea tu, bali kwa kuheshimu mamlaka yake kwa kutenda mema.

Ujumbe wa kuzaliwa kwa Yesu ni tangazo la wokovu kwa mwanadamu. Tunachotakiwa ni kumkaribisha akae kwetu. Yaani tumpokee afanye makao mioyoni mwetu. Amina

Tunakutakia ibada njema ya usiku Mtakatifu.

 

Heri Buberwa Nteboya 

Mlutheri

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com

Butainamwa, Bukoba