Date: 
19-08-2025
Reading: 
1 Samweli 15:24-31

Jumanne asubuhi tarehe 19.08.2025

1 Samweli 15:24-31

24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.

25 Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana.

26 Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.

27 Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.

28 Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.

29 Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute.

30 Akasema, Nimekosa; lakini uniheshimu sasa, nakuomba, mbele ya wazee wa watu wangu, na mbele ya Israeli, rudi pamoja nami, nimwabudu Bwana, Mungu wako.

31 Basi Samweli akarudi na kuandamana na Sauli; naye Sauli akamwabudu Bwana.

Tuenende kwa hekima ya Mungu;

Sauli baada ya kutawazwa kuwa Mfalme alitawala pasipo kumpendeza Bwana. Hakufuata maelekezo ya Bwana aliyemtawaza kuwa Mfalme ili awaongoze watu wake. Hilo linadhihirika Bwana anapompa ujumbe Samweli akimtuma kwa Sauli. 

Angalia ujumbe wa Bwana akimtuma Samweli kwa Sauli;

1 Samweli 15:10-11

10 Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema,
11 Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha.

Samweli aliupeleka ujumbe wa Bwana kwa Sauli, na somo la asubuhi hii ni itikio la Sauli akiomba kusamehewa ili apate kumwabudu Bwana. Sauli alimg'ang'ania Samweli hadi akafanya toba na kumwabudu Bwana. Sauli aliongozwa na hekima ya Mungu akatubu. Tukiongozwa na hekima ya Mungu maisha yetu yanakuwa ya toba daima, maana kwa njia ya toba tunapokea msamaha wa dhambi na kuurithi uzima wa milele. Amina

Uwe na siku njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com