Date: 
17-07-2025
Reading: 
Yuda 1:17-23

Alhamisi asubuhi tarehe 17.07.2025

Yuda 1:17-23

17 Bali ninyi, wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo,

18 ya kwamba waliwaambia ya kuwa, Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa zao wenyewe za upotevu.

19 Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na Roho.

20 Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,

21 jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele.

22 Wahurumieni wengine walio na shaka,

23 na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.

Tuhurumiane katika Kristo;

Tumesoma sehemu ya waraka wa Yuda ambao una sura moja, ambapo Yuda anatoa maonyo na mahimizo. Yuda anawaandikia wasomaji wake kukumbuka maneno ya mitume wa kale wa Kristo, kwamba watakuwepo watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa zao. Yuda anasema watu hao ndiyo waletao matengano, yaani jamii isiyo pamoja. Yuda anaandika kuhusu kujilinda katika upendo wa Mungu kwa kumtegemea Kristo.

Yuda anakazia kuingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo hata uzima wa milele, akisema tuwahurumieni wengine walio na shaka. Ujumbe wa Yuda kwa Kanisa la leo ni kila mmoja kuishi akimhurumia mwenzake katika Yesu Kristo, ili tukae kwa pamoja kama Kanisa la Mungu. Kama tunavyohurumiwa na Kristo, nasi tuhurumiane kama tunavyoagizwa katika utume wetu. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa