Date: 
16-07-2025
Reading: 
Luka 6:36-38

Jumatano asubuhi tarehe 16.07.2025

Luka 6:36-38

36 Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

37 Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.

38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

Tuhurumiane katika Kristo;

Yesu anafundisha akisema yeye anayo huruma, hivyo kuwataka wanafunzi wake kuwa na huruma kama yeye. Anawaelekeza kutohukumu ili wasihukumiwe. Wasilaumu ili wasilaumiwe. Anawaambia kuachilia ili waachiliwe. Yesu anaendelea kuwaambia wanafunzi wake kuwa watoaji kwa upendo, na kuwa wema kwa watu wote.

Ukiangalia neno hili tulilosoma, Yesu anawafundisha wanafunzi wake kuwa na huruma kwa wengine. Anawafundisha kuishi na watu kwa kuwa tayari kuwasamehe, kuwapokea na kuwasaidia. Ndiyo wito ambao juma hili tunapewa, kuwa na huruma miongoni mwetu, tukisaidiana katika safari ya imani ili sote kwa pamoja tuwe na mwisho mwema. Amina

Siku njema

Heri Buberwa