Date: 
15-07-2025
Reading: 
Luka 6:6-11

Jumanne asubuhi tarehe 15.07.2025

Luka 6:6-11

6 Ikawa siku ya sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza.

7 Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia.

8 Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama.

9 Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?

10 Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena.

11 Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.

Tuhurumiane katika Kristo;

Yesu anaingia hekaluni siku ya sabato na kumponya mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. Waandishi na Mafarisayo walipata shida na uponyaji siku ya sabato. Lakini Yesu akitambua mawazo yao, anawauliza kama ni halali kutenda mema au mabaya, kuponya au kuangamiza siku ya Sabato. Hawakumjibu kitu, Yesu akamwambia aliyepooza anyooshe mkono, akapona mara.

Waandishi na Mafarisayo walikuwa wakitawaliwa na mawazo ya Agano la Kale, kuitunza Sabato. Hawakujua na kuamini kuwa Yesu ndiye Bwana wa sabato mwenye amri juu ya vitu vyote kama alivyokuwa amewaambia kabla;

Luka 6:5

Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.

Yesu hakuangalia mawazo ya waaandishi na Mafarisayo, bali huruma yake ilimfanya amponye aliyepooza mkono. Ni kwa mfano huo, nasi tunaalikwa kuwa na huruma miongoni mwetu ili tumshuhudie Kristo katika kweli yake. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa