Jumatatu asubuhi tarehe 14.07.2025
Matendo ya Mitume 16:16-18
16 Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.
17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.
18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.
Tuhurumiane katika Kristo;
Asubuhi hii tunasoma sehemu ya habari ya Paulo na Sila kufungwa gerezani. Paulo akiwa na Sila alimuombea kijakazi aliyekuwa na pepo wa uaguzi akamtoka. Sasa waliokuwa wanamtumia yule kijakazi ndiyo wakachukia, wakaamuru Paulo na Sila wapigwe na kutupwa gerezani. Wakiwa gerezani usiku walimsifu Mungu, milango ikafunguka wakatoka.
Katika somo hili;
1. Huruma ya Mungu ilikuwa juu ya kijakazi aliyeombewa na pepo la uaguzi likatoka.
2. Huruma ya Mungu ilikuwa juu ya Paulo na Sila, waliofungwa gerezani na kutolewa usiku huo huo
3. Huruma ya Mungu ilikuwa juu ya mlinzi wa gereza walimofungwa Paulo na Sila, ambaye baada ya kuona matendo makuu ya Mungu alibatizwa yeye na familia yake usiku uleule.
Tunakumbushwa kumtumaini Bwana atuwezeshaye na kuturehemu siku zote, lakini nasi tukipendana na kuhurumiana katika Kristo Yesu. Tukiwa na huruma tutahurumiwa kama Yesu alivyosema;
Mathayo 5:7
Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.Amina
Tunakutakia wiki njema yenye huruma ya Mungu.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650