Date: 
05-07-2025
Reading: 
Luka 14:16-24

Jumamosi asubuhi tarehe 05.07.2025

Luka 14:16-24

16 Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,

17 akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.

18 Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.

19 Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.

20 Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.

21 Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.

22 Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.

23 Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.

24 Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.

Wito wa kuingia Ufalme wa Mungu;

Ni mfano wa mtu aliyefanya karamu kubwa na kualika watu wengi. Muda ulipofika alimtuma mtumwa wake kuwakaribisha waalikwa, maana karamu ilikuwa tayari. Walitoa udhuru mmoja baada ya mwingine. Wa kwanza alisema anaenda shambani kwake, mwingine alisema anakwenda kujaribu ng'ombe aliokuwa amewanunua, mwingine alikuwa ndiyo kwanza ameoa, akasema hawezi kufika! Bila shaka udhuru ulikuwa mwingi kwa wasiofika.

Yule mwenye nyumba alikasirika sana akaagiza waletwe vipofu, viziwi, maskini na viwete kula karamu. Hawakujaa ukumbini. Ikaamriwa waletwe watu wote barabarani na mipakani. Mfano huu wa Yesu leo ni wa watu wanaohubiriwa Injili lakini hawaamini, hawampokei Yesu. Bado wana sababu tele, za kwa nini hawawezi kuja kwa Yesu hadi wakamilishe mambo fulani. Wakati ni sasa, mwamini Yesu uingie katika Ufalme wake. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa