Date:
02-01-2025
Reading:
Luka 4:16-18
Alhamisi asubuhi tarehe 02.01.2025
Luka 4:16-18
16 Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.
17 Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa,
18 Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,
Anza yote katika jina la Yesu Kristo;
Yesu alikuwa anasoma kutoka Isaya 61:1-2. Nukuu ya Luka ni tafsiri kama ilivyoandikwa katika Kihebrania, pia sawa na Kiyunani. Tofauti ni kuwa Luka anaongeza maneno "kuwaacha huru wafungwa waliosetwa" (mwisho wa mstari wa 18) maneno ambayo yanatoka Isaya 58:6. Yesu anaeleza kutimilika kwa mstari huu, kama tutakavyoona.
Roho Mtakatifu alimshukia Yesu wakati akibatizwa. Mungu wetu katika Utatu yu katika utaratibu wa nafsi moja kamili. Hakuna mgawanyo kati ya mapenzi ya Baba, mapenzi ya mwana, au mapenzi ya Roho Mtakatifu. Kazi ya kila nafsi yaweza kuwa tofauti, kwa sababu Mungu anazo nafsi tatu, kwamba Mwana ndiye aliyesulibishwa (siyo Baba), Roho Mtakatifu ndiye aliyewashukia Mitume siku ya Pentekoste (siyo Baba wala Mwana), wote wakifanya kazi kwa pamoja. Roho Mtakatifu alikuwa, na yuko na Yesu. Hapa Mungu alikuwa akionyesha Yesu anavyochukua ofisi ya ufunguo (rejea shule ya kipaimara kuhusu ofisi ya ufunguo) hapa duniani, maana alitoka mbinguni. Chochote alichohubiri Yesu lilikuwa neno la Mungu.
Kuwahubiria maskini habari njema;
Maskini ni nani? Luka anatumia lugha hii kuliko Injili nyinginezo, na mara zote Yesu anawaongelea wasio na kitu. Haimaanishi watu wasio na fedha, au wasio na kitu kabisa. Yesu anamaanisha wasiotubu. Anayetubu ni maskini kwa maana kuwa hakuna kitu unaweza kulipa ili usamehewe na Bwana. Yesu ndiye mtoaji, sisi wapokeaji. Yesu ndiye hutusamehe, pale tunapotubu.
Kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao;
Hili ni jambo lilelile, yaani uhuru kwa waliosetwa ni Injili kwa maskini. Hawa ni waliofungwa dhambini na kustahili adhabu ya milele. Tunapobatizwa tunazaliwa upya, na tunaingizwa katika orodha ya warithi wa uzima wa milele. Tunafunguliwa.
Vipofu kuona tena;
Andiko la Kihebrania kwa sehemu hii linasema "kuwatoa wafungwa gizani". Yesu aliponya vipofu wengi, hata wale vipofu tangu kuzaliwa. Lakini hapa aaongelea upofu wa kiroho kama alivyosema;
Yohana 9:39
Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.Yesu alimaanisha Mafarisayo walioona kuwa vipofu wa kweli yake, kwa sababu ya majivuno na kutokuamini.
Kama waamini tumfuate Yesu ili kuondoa upofu. Lakini tuwasaidie wengine kwa kuwafundisha kweli ya neno lake, ili waone wasiwe vipofu.
Kuwaacha huru waliosetwa;
Neno hili linatoka Isaya 58:6, lakini wazo liko Isaya 61 kuanzia mstari wa 1 ambapo haijatafsiriwa hapa, lakini ni "waliovunjika moyo".
Wakati wa Yesu watu waliumizwa sana na utawala. Wajane na yatima walikuwa daraja la watawala kuneemeka. Mifumo ya kodi haikuwa rafiki. Leo, waliosetwa, waliovunjika moyo ni wale wanaokumbana na mateso ya shetani, dunia na mwili wetu. Leo hii, dunia imebadilika kwa kiwango cha baadhi ya vitu na mifumo kuwa maadui wa ufalme wa Mungu. Mungu anataka tuwe makini na dunia. Tutambue wapi tumekosa na kutubu. Yesu anatangaza kutuweka huru, akitutangazia msamaha wa dhambi pale tulipokosa, akitupa ahadi ya uzima wa milele.
Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa;
Huu ulikuwa mwaka wa Jubilee kutoka kwenye kalenda ya Agano la kale, mwaka wa hamsini ambapo madeni yote yalifutwa na wafungwa wote kuachiwa huru. Ardhi na mali iliyouzwa ilirudishwa kwa familia husika (Soma Mambo ya Walawi 25). Unabii wa Isaya 61 unakuja na habari ya Yesu kuweka watu huru.
Tukitafakari ujumbe huu tunaona kuwa sisi kama wafuasi wa Yesu tunahitaji kuwaambia wengine kuhusu Yesu, na kwa kufanya hivyo tunatangaza kuwa;
2 Wakorintho 6:2
(Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)Mwaka uliokubaliwa ni pale tunapowekwa huru. Ni pale tunapompokea Yesu atuokoe na kutuongoza. Tuadhimishe jubilee ya ubatizo wetu, maana kupitia ubatizo tumefunguliwa milele. Hii ni jubilee ya milele.
Mwisho;
Tunapoanza mwaka huu wa 2025, Yesu Kristo anatuletea habari njema ya wokovu. Anatutangazia uhuru toka dhambini, anatufanya tuone na kuturudishia tulivyonyang'anywa.
Mungu anaahidi kuwa nasi katika mwaka huu wote, wajibu wetu ni kupokea tangazo kama ambavyo Yesu amelitangaza leo.
Uhuru upo kwa ajili yako, mpokee Yesu akufungue, ili mwaka huu uwe wa baraka kwako.
Tunakutakia mwaka mzuri wa 2025 wenye ushuhuda na mafanikio.
Heri Buberwa
0784 968650