Date: 
29-07-2024
Reading: 
Hesabu 14:18-20

Jumatatu asubuhi tarehe 29.07.2024

Hesabu 14:18-20

18 Bwana ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne.

19 Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa.

20 Bwana akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa;

Mungu hupendezwa na mwenye moyo wa toba;

Tunasoma wana wa Israel wakiwa njiani kuelekea nchi ya ahadi. Pamoja na Mungu kutuma wapelelezi na kuleta habari ya nchi njema waliyokuwa wanaiendea, bado Israel walitamani kurudi Misri. Jambo hili lilimchukiza Bwana hadi akaamua kuwaadhibu kama anavyomwambia Musa;

Hesabu 14:11-12

11 Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.
12 Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao.

Musa aliwaombea Israel msamaha kwa Mungu, kwamba awasamehe uovu wao, kama alivyowasamehe tokea Misri. Somo tulilosoma ni mwendelezo wa sala ya Musa akiomba Israel wasamehewe, na mstari wa 20 ni Mungu anawasamehe. 

Tunakumbushwa kuwa Mungu hutusamehe dhambi zetu pale tunapotambua tumekosa tukajuta na kutubu. Maisha ya imani ya kweli, toba na msamaha hutuweka kwa Kristo ambaye hutuongoza daima hata uzima wa milele. Amina

Tunakutakia wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.

Heri Buberwa