Date: 
10-04-2024
Reading: 
Wakolosai 1:16-17

Jumatano asubuhi tarehe 10.04.2024

Wakolosai 1:16-17

16 Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.

17 Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.

Tutunze mazingira yetu;

Mtume Paulo anamtaja Kristo kama msingi wa Imani iletayo tumaini kwao waaminio. Huyu ndiye aliyetuokoa na kutuingiza katika Ufalme wa Mungu. Kristo huyu ndiye katika yeye vitu vyote viliumbwa, vinavyoonekana na visivyoonekana. Paulo anasisitiza kuwa vitu vyote viliumbwa kwa njia yake.

Mtume Paulo anasema Kristo alikuwapo kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Angalia msisitizo wa Paulo kwa Kristo aliye juu ya vyote;

Wakolosai 1:18-20

18 Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.
19 Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae;
20 na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.

Ujumbe wa Paulo leo asubuhi ni kwamba Kristo yuko juu ya vitu vyote. Uumbaji wote ni wa kwake kama Mungu kweli, na kwa njia hii anatuita kumwamini yeye aliye juu ya vyote, siku zote za maisha yetu. Amina

Jumatano njema 

Heri Buberwa