Date: 
09-04-2024
Reading: 
Kumbukumbu la Torati 23:9-25

Jumanne asubuhi tarehe 09.04.2024

Kumbukumbu la Torati 23:9-25

9 Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika marago, jilinde na kila neno baya.

10 Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo;

11 lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo.

12 Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje;

13 nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho;

14 kwa kuwa Bwana. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha.

15 Usimrudishe kwa bwana wake mtumwa aliyejiponya kutoka kwa bwana wake kuja kwako;

16 na akae nawe, katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, mahali atakapochagua palipo pema machoni pake; usimwonee.

17 Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.

18 Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili.

19 Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba;

20 mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.

21 Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.

22 Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.

23 Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.

24 Uingiapo katika shamba la mizabibu la jirani yako, utaweza kula zabibu za kukushibisha, kama upendavyo; ila usitie katika chombo chako.

25 Uingiapo katika mmea wa jirani yako waweza kuyapurura masuke kwa mkono wako; ila usisongeze mundu katika mmea wa jirani yako.

Tutunze mazingira yetu;

Sura ya 23 ya kitabu cha Kumbukumbu la Torati huanza na aina ya watu ambao hawakuruhusiwa kukwepo kwenye kusanyiko la Bwana. Ndiyo, wapo watu ambao Musa hakutaka wawepo kwenye kusanyiko. Ni Waamoni na Wamoabu hawakuruhusiwa kuingia kwenye ushirika, kwa sababu hawakuwasaidia wana wa Israeli walipotoka Misri. Hawakuwapa chakula wala kuwajali kwa lolote.

Hao watu ambao hawakuwajali Israeli walielekezwa kutowachukia Taifa la Mungu (Israeli). Musa anaonekana akitoa maelekezo kwa sababu Mungu alikuwa kati ya watu wake wakati wote. Musa anawafundisha wema, pale anapowafundisha ujirani mwema katika maisha yote.

Mstari wa 24 unafundisha kutimiza wajibu kwa Bwana na watu, wakati mstari wa 24 na 25 inaelekeza kuishi na kutenda mema kwa jirani.

Musa alikuwa akitoa maelekezo aliyopewa na Bwana, kwamba watu waishije. Hapa alikemea watu wenye chuki wasitokee kwenye kusanyiko. Maana yake ni kuwa Mungu alichukia matendo yao ya kuwachukia Israeli.

Kwa sisi leo, Mwokozi wetu Yesu Kristo hutufundisha kutenda mambo yote kwa Utukufu wa Mungu, ili tuwe na mwisho mwema katika yeye. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa