Date: 
01-03-2024
Reading: 
Waefeso 4:1-3

Hii ni Kwaresma 

Ijumaa ya tarehe 01.03.2024

Siku ya maombi ya dunia

Zab 41:1-4

1Kor 16:13-14

*Efe 4:1-3

Waefeso 4:1-3

1 Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;

2 kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;

3 na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

Mchukuliane katika upendo;

Sura ya kwanza hadi ya tatu ya waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso ni maelezo kuhusu imani wakati sura ya nne hadi ya sita ni matokeo ya imani husika katika maisha kwa waaminio. Somo letu ambalo ni sehemu ya waraka huu, linayo maudhui ya umoja katika Kanisa. Huu ndiyo mtazamo hasa wa somo hili. 

Mtume Paulo anaanza waraka huu kwa kuwakumbusha wasikilizaji/wasomaji wake kwamba yeye ni mfungwa katika Bwana (1). Ingawaje, anaonesha kuwa kuwa kwake mfungwa hakumuondoi kwenye njia sahihi. Ndiyo maana anajiita mfungwa katika Bwana. Tunaweza kufikiria kufungwa kunavyopoteza muda kwa sababu ya kumnyima uhuru mfungwa husika. Lakini Paulo mtazamo wake ni tofauti. Kufungwa kwake hakumzuii kuendelea na utume wake. Mahali pengine anawaeleza Wafilipi kufungwa kwake ni kwa ajili ya kuhubiri Injili;

Wafilipi 1:12-14

12 Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa kuieneza Injili;
13 hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia.
14 Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, hali wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu.

Hadi hapa napata mafunzo mawili;

 1. Tusiitilie shaka nguvu ya Kristo mahali popote tuwapo;

Hali ya Paulo kufungwa inatukumbusha mazingira ya maisha yetu kutotutenga na Kristo. Paulo anadhihirisha kwamba nguvu ya Kristo haizuiliwi na jambo lolote iwapo amwaminiye humpa maisha yake na kumtegemea. Yesu mwenyewe alituhumiwa kwa kukaa na kula na wenye dhambi, haikuondoa Utukufu wake. Ni kama Paulo alivyofungwa, bado akaendelea kuwa Paulo yule yule. Katika hali yoyote tunayokuwemo, tukimtegemea Kristo tunashinda yote.

 

2. Tafakari na maisha ya imani haina mwisho. 

 Barua za Mtume Paulo akiwa kifungoni (kama Waefeso na Wafilipi) ni tafakari ya maana ya imani katikati ya maumivu. Hapa upo msisitizo wa Paulo kutimiza wajibu wetu hapa duniani ipasavyo. Yaani hapo juu (no 1) tumeona kwamba njia zetu zisitutenge na Kristo, sasa hapa tunaambiwa kuwa kutotengwa na Kristo iwe hali ya kudumu. 

Mtume Paulo hapa anatuandikia mtu mmoja kama waaminio, lakini pia kama Kanisa la Mungu, yaani wote kwa pamoja. Ndiyo maana mistari wa pili anatusihi kuwa wanyenyekevu, wapole, wavumilivu, lakini tukichukuliana kwa upendo. Kumbe upo ujumbe wa kuwa na imani katika Kristo Yesu, tukiishi kwa upendo na amani. 

Dhana nzima ya kufungwa katika Kristo ni kuwa na imani katika yeye, tukikaa pamoja kwa upendo na unyenyekevu. Ukisoma mbele zaidi unaona jinsi Paulo anavyosisitiza waamini kukaa pamoja na kuujenga mwili wa Kristo;

Waefeso 4:15-16

15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.
16 Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.

Mchukuliane katika upendo;

Paulo anaangazia Kanisa kuwa mwili wa Kristo. Paulo anasema mwili unacho kiungo chenye akili, kwa maana nyingine ni muhimu kwetu waamini kujua nini tunaamini, na kwa nini tunaamini hivyo. Sababu mojawapo ni kuwa tunaishi katika zama ambazo uongo unaaminika kwa urahisi, kwa sababu ya baadhi yetu kutaka njia za mkato katika mafanikio. Hapa ndipo Mtume Paulo anasisitiza kuongea ukweli katika upendo;

Waefeso 4:15

Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.

Hivyo ushuhuda wetu katika kweli ufungwe katika unyenyekevu, upole, umoja, lakini muhimu zaidi Upendo (2). 

Tuwe na Imani ya kweli na umoja katika Kristo mfufuka aliye Mwokozi wetu, leo na siku zote. Amina.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com