Date: 
27-11-2023
Reading: 
Yohana 13:19-20

Jumatatu asubuhi tarehe 27.11.2023

Yohana 13:19-20

19 Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye.

20 Amin, amin, nawaambieni, Yeye ampokeaye mtu ye yote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi; ampokea yeye aliyenipeleka.

Maandalizi ya uzima wa milele;

Neno tulilosoma ni sehemu ya maneno ya Yesu kwa wanafunzi wake, siku ile alipofanya karamu ya mwisho. Alikuwa anaawaambia yatakayompata, kwa jinsi alivyokuwa akikiendea kifo. Sehemu tuliyosoma inaeleza jinsi ilivyo heri kumpokea yule aliye mjumbe wa Kristo, maana humshuhudia Kristo mwenyewe. Yule ampokeaye Kristo, ampokea Mungu mwenyewe.

Ujumbe wa Yesu hapa unahusu kumpokea yeye kama Bwana na Mwokozi wa ulimwengu. Tukilisikia neno lake na kuliamini, basi tunampokea yeye Yesu Kristo. Neno lake hutuwezesha kuishi kadri apendavyo, na hatimaye kuurithi uzima wa milele. Kumwamini Yesu ni maandalizi kwa uzima wa milele. Amina.

Uwe na wiki njema.

Heri Buberwa