Date: 
01-11-2023
Reading: 
1 Wakorintho 3:16-17

Jumatano asubuhi tarehe 01.11.2023

1 Wakorintho 3:16-17

16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

Tutengeneze mambo yaliyoharibika;

Jana asubuhi tuliona Mtume Paulo akiandika ya kuwa msingi imara katika imani yetu ni Yesu Kristo. Kwamba katika maisha yetu, tegemeo la mambo yote ni Imani katika Kristo. Sasa katika msingi huo, asubuhi ya leo Mtume Paulo anasema miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, na Mungu anakaa ndani yetu. Aharibuye hekalu ataharibiwa maana hekalu la Mungu ni takatifu ambalo ni sisi.

Tunaishi maisha ya Imani rohoni, lakini roho iko mwilini. Kwa hiyo hakuna mwili bila roho. Paulo anapozungumzia miili kuwa hekalu la Roho Mtakatifu, anatukumbusha kuwa mfumo mzima wa maisha kwa kila aaminye lazima uwe ni katika kumtazama Kristo. Kwa maana hiyo lazima Roho Mtakatifu akae mioyoni mwetu, atuwezeshe kumcha Bwana na kutenda yatupasayo kuelekea uzima wa milele. Amina.

Jumatano njema.

Heri Buberwa