Date: 
10-10-2023
Reading: 
Mathayo 15:10-20

Jumanne asubuhi tarehe 10.10.2023

Mathayo 15:10-20

10 Akawaita makutano akawaambia

11 Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi.

12 Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa?

13 Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.

14 Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.

15 Basi Petro akajibu, akamwambia, Tueleze mfano huo.

16 Yesu akasema, Hata sasa ninyi nanyi mngali hamna akili?

17 Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?

18 Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano;

20 hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi.

Uhuru wa Mkristo;

Mafarisayo na waandishi walimuuliza Yesu ni kwa nini wanafunzi wake hawakuheshimu wazee, maana hawakunawa ilivyostahili. Yesu naye akawajibu kwa nini hawakutii amri za Mungu kwa sababu ya mapokeo. Walichukia sana, na hili ndilo jambo ambalo tumelisoma kwenye ujumbe wa leo asubuhi. Yesu anawaita waandishi na mafarisayo vipofu ambao ni viongozi wa vipofu. Hii ni kwa sababu yao ya kushikilia sheria na mapokeo, na siyo Injili ya kweli kama aliyohubiri Kristo.

Waandishi na Mafarisayo walishikilia mapokeo badala ya kumsikiliza Yesu na kumwamini, maana Yesu ndiye alikuwa utimilifu wa torati. Hadi hapa Mafarisayo na waandishi walikuwa gizani. Walikuwa dhambini, hawakuwa huru.

Sisi tumewekwa huru na Kristo Yesu kwa njia ya kifo msalabani. Tunakumbushwa kudumu katika Imani hii kwa msaada wa Mungu ili tuwe na mwisho mwema. Amina.

Jumanne njema.

 

Heri Buberwa