Date: 
27-09-2023
Reading: 
Matendo 12:5-11

Jumatano asubuhi tarehe 27.09.2023

Matendo ya Mitume 12:5-11

5 Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.

6 Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza.

7 Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi.

8 Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate.

9 Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono.

10 Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha.

11 Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.

Mungu amejaa huruma;

Baada ya Herode kumuua Yakobo (ndugu yake Yohana) anaamuru Petro afungwe gerezani. Petro anafungwa gerezani akilala katikati ya askari, hadi Pasaka iishe. Bwana alimtuma malaika wake akamwondoa Petro gerezani usiku, pamoja na kulindwa na askari wengi. Petro alitoka gerezani akaungana na jamaa yake tena. Herode baadaye alijipa utukufu akaliwa na chango, akafa.

Petro alikuwa anafanya kazi katika mazingira magumu. Fikiria hadi kufungwa gerezani! 

Lakini Mungu alikuwa naye. Mungu alikuwa na huruma kwa Petro, lakini pia kwa taifa lake ili Petro azidi kuhubiri Injili. Petro alimtegemea Mungu katika kazi yake, na Mungu akamuongoza katika hatua zote. Nasi tukimtegemea Kristo tutashinda. Amina.

Jumatano njema.

Heri Buberwa