Date: 
25-09-2023
Reading: 
Mwanzo 19:1-14

Jumatatu asubuhi tarehe 25.09.2023

Mwanzo 19:1-14

1 Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi.

2 Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha.

3 Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala.

4 Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote.

5 Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua.

6 Lutu akawatokea mlangoni, akafunga mlango nyuma yake.

7 Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi.

8 Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mtu mume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu.

9 Wakasema Ondoka hapa! Kisha wakanena, Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, anataka kuhukumu! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa. Wakamsonga sana huyo mtu, huyo Lutu, wakakaribia wauvunje mlango.

10 Lakini wale watu wakanyosha mikono yao, wakamwingiza Lutu kwao nyumbani, wakaufunga mlango.

11 Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakachoka kwa kuutafuta mlango.

12 Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa;

13 maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za Bwana; naye Bwana ametupeleka tupaharibu.

14 Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu Bwana atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze.

Mungu amejaa huruma;

Asubuhi hii tunasoma Mungu akituma ujumbe wake nyumbani kwa Lutu. Malaika wawili walifika kwa Lutu akawakaribisha vizuri. Wenyeji wa Sodoma waliwataka wale wageni ili "wawajue" usiku ule ule! Hakika uovu ulizidi katika Sodoma na Gomora! Unajua walitaka nini hao watu wa Sodoma usiku ule? 

Walisema "tupate kuwajua" 

Angalia walichokitaka maana yake;

Mwanzo 4:1, 17, 25
1 Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.
17 Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe.
25 Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.

Sasa nafikiri unaweza kuona maana ya jibu alilowapa Lutu;

Mwanzo 19:7-8

7 Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi.
8 Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mtu mume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu.

Kumbe walitaka kuwadhuru wageni wa Lutu, na kuwatenda ubaya. 

Hawa watu waliozingira nyumba ya Lutu wakiwataka wageni ni watu waliokuwa waovu. Ukiendelea kusoma unaona kuwa malaika wale walimuondoa Lutu Sodoma, halafu moto ukashuka kuiangamiza Sodoma na Gomora. Watu wa Sodoma na Gomora waliangamizwa kwa moto kwa sababu ya uovu.

Lakini Lutu hakuangamia kwa sababu alikuwa mwenye haki mbele za Mungu. Huruma ya Mungu ilikuwa juu yake.

Huruma ya Mungu iko kwa watu wote, ndiyo maana anatupa nafasi ya kutubu na kumrudia yeye. Tukitubu dhambi anatusamehe na kutupa uzima wa milele. Amina.

Tunakutakia wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.

Heri Buberwa