Date: 
14-08-2023
Reading: 
Zaburi 38:1-7

Jumatatu asubuhi tarehe 14.08.2023

Zaburi 38:1-7

1 Ee Bwana, usinilaumu katika ghadhabu yako, Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako.

2 Kwa maana mishale yako imenichoma, Na mkono wako umenipata.

3 Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu.

4 Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno.

5 Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu.

6 Nimepindika na kuinama sana, Mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika.

7 Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu.

Mithali 14:34

Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.

Inaaminika kwamba Zaburi ya 38 aliiandika Daudi baada ya kumuua Uria. Zaburi nyingine ni 32 na 51. 

Habari ya kumuua Uria inapatikana katika kitabu cha pili cha Samweli sura ya 11. Daudi alimuona mwanamke mzuri akatamani kumuoa, lakini mwanamke huyo Betsheba alikuwa mke wa mtu, Uria aliyekuwa askari. 

Wakati huo jeshi lilikuwa kwenye mapigano, Daudi akaelekeza Uria atangulizwe mbele, akapigwa akafa. Baada ya Uria kufa, Daudi akamuoa Betsheba. Mungu hakupendezwa na jambo hili, akamtuma Nathani kumpa Daudi ujumbe kwamba hakufanya sahihi kumuua Uria ili amuoe Betsheba. Daudi alitubu, na Mungu alimsamehe.

Hadi hapa;

Inaaminika kuwa Daudi aliandika Zaburi hii ya 38 akisubiri msamaha toka kwa Mungu. Daudi alisikitika sana kwa ujio wa Nathani, na aliumwa baada ya kuupokea ujumbe wa Mungu toka kwa Nathani. Daudi aliamini aliumwa kwa sababu hii, kama mstari wa tatu na ule wa saba inavyosomeka;

Zaburi 38:3, 7

3 Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu.
7 Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu.

Katika Zaburi hii Daudi anamtazama Mungu kumsamehe dhambi baada ya kutambua alivyokosa na kutubu, baada ya kutotenda haki kwa Uria. Zaburi hii inatukumbusha kumtazama Yesu Kristo aliye Mwokozi wetu, tukitenda haki katika jamii yetu kwa Utukufu wake. Amina.

Uwe na wiki njema ukitenda haki.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com