Date: 
22-07-2023
Reading: 
Mathayo 22:34-40

Jumamosi asubuhi tarehe 22.07.2023

Mathayo 22:34-40

34 Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja.

35 Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu;

36 Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?

37 Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

39 Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

40 Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.

Amri ya Upendo;

Masadukayo hawakuamini katika ufufuo. Walimuuliza Yesu kwamba mke aliyeolewa na wanaume saba, mume wake atakuwa yupi kati ya wale saba siku ile ya ufufuo? Yesu akawajibu kuwa mbinguni hakuna kuoa wala kuolewa, na pia Mungu ni wa walio hai, siyo wafu. Kwa lugha ya leo tungesema Masadukayo wakawa "wapole".

Sasa ndipo tunakuja kwa somo letu, Mafarisayo na Masadukayo wakapatana kwa pamoja. Mwanasheria mmoja akamuuliza Yesu, amri iliyo kuu ni ipi? Bila shaka kwa sababu alikuwa mwanasheria walidhani angekuwa mtu sahihi kumkamata Yesu kwa mafundisho ya uongo kama walivyomtuhumu wale Mafarisayo na Masadukayo.

Yesu alijibu kwamba amri kuu ni Upendo. Kumpenda Mungu ikiwa ya kwanza, na kumpenda jirani kama nafsi yako, ikiwa ya pili. Msisitizo wa Yesu ni kuwa amri kuu ni Upendo.

Basi Yesu kama Yesu alivyosema kuwa amri kuu ni upendo, tupendane. Amina.

Jumamosi njema 

Heri Buberwa