Date: 
04-07-2023
Reading: 
Ayubu 32:6-12

Jumanne asubuhi tarehe 04.07.2023

Ayubu 32:6-12

6 Basi Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, akajibu, na kusema, Mimi ni kijana, na ninyi ni wazee sana; Kwa hiyo nilijizuia, nisithubutu kuwaonyesha nionavyo.

7 Nilisema, Yafaa siku ziseme, Na wingi wa miaka ufundishe hekima.

8 Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.

9 Sio wakuu walio wenye akili, Wala sio wazee watambuao hukumu.

10 Basi nilisema, Nisikilizeni mimi; Mimi nami nitawaonyesha nionavyo.

11 Tazama, niliyangojea maneno yenu, Nilizisikiliza nisikie hoja zenu, Hapo mlipokitafuta mtakalonena.

12 Naam, niliwasikiza ninyi, Na tazama, hapana mmoja aliyemshinda Ayubu, Wala kumjibu maneno yake, kati yenu.

Kijana uwe hodari katika Imani;

Baada ya Ayubu kupitia mateso mengi alikuwa na hoja nyingi sana. Katika hoja hizo anaelezea ukuu wa Mungu na kuonekana mnyenyekevu katika hali zote. Hoja zake zilikuwa nzito, ndiyo maana katika somo la asubuhi hii tunamuona Elihu, mtu aliyeshindwa kuzijibu, na wazee aliowategemea walishindwa kuzijibu hoja za Ayubu.

Ayubu alikuwa akimtukuza na kumuelezea Bwana. Kutambua hoja za Ayubu kulihitaji msaada wa Mungu. 

Vijana leo tusidhani tunaweza kujua kila kitu. Tusome sana, tutafiti, tuulize, tujifunze kwa wengine. Lakini muhimu kuliko yote tumtegemee Mungu katika njia zetu. Tuwe hodari katika Imani. Amina.

Siku njema.

Heri Buberwa