Date: 
15-06-2023
Reading: 
Wafilipi 1:21-26

Alhamisi asubuhi tarehe 15.06.2023

Wafilipi 1:21-26

21 Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.

22 Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui.

23 Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana;

24 bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu.

25 Nami nikitumaini hayo, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, ili mpate kuendelea na kufurahi katika imani;

26 hata mzidi kuona fahari katika Kristo Yesu juu yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi tena.

Mungu au Ulimwengu;

Mtume Paulo anaandika juu ya kuishi na kufa kwake, kwamba akiishi ni Kristo na akifa ni faida. Katika kuishi kwake anatamani kwenda akakae na Kristo, na hiyo inawezekana mtu akiishi katika kumwamini na kumfuata Kristo. Paulo anawasihi Wafilipi kudumu katika Kristo wakimwabudu katika roho na kweli ili wafe katika yeye (Kristo).

Paulo anaposema kuishi ni Kristo na kufa ni faida anamchagua Mungu. Anaonesha kuwa akiishi na kufa katika Kristo anaenda kukaa na Kristo milele. Hakikisha unaishi katika Kristo, ufe katika Kristo, ili ukakae na Kristo. Chagua Mungu, na siyo Ulimwengu ili uurithi uzima wa milele. Amina.

Alhamisi njema.

 

Heri Buberwa 

Mlutheri