Date: 
14-06-2023
Reading: 
Matendo ya Mitume 5:34-42

Jumatano asubuhi tarehe 14.06.2023

Matendo ya Mitume 5:34-42

34 Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo,

35 akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa.

36 Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu.

37 Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika.

38 Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa,

39 lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.

40 Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao.

41 Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.

42 Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.

Mungu au Ulimwengu;

Sura ya tano inaanza kwa kuonesha kazi ya Mitume hekaluni, ambapo Anania na Safira walileta sadaka wakiwadanganya mitume kwamba ni sadaka kamili. Walikufa hapo hapo hekaluni. Habari hizi zilienea, Mitume wakafungwa gerezani.

Mungu aliwatoa gerezani wakaenda hekaluni wakiendelea kufundisha. Ndipo wale Mitume wakaitwa barazani wakiambiwa waache kufundisha habari za Yesu. Mitume wakasema imewafaa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Yaani walichagua kuhubiri Injili kwa gharama yoyote.

Sasa ndipo asubuhi hii tunamsoma Farisayo Gamalieli akisimama na kuwasihi wazee wa baraza waachane na hawa Mitume, maana kwa kuwafukuza na kuwatesa Mitume wanashindana na Mungu. Basi wakawachukua Mitume wakawapiga, wakawaamuru waondoke na wasinene katika jina la Yesu. Mitume walifurahi kuaibishwa kwa ajili ya Kristo na hawakuacha kuhubiri.

Farisayo Gamalieli alitambua kuwa Mitume walihubiri Injili ya kweli, hivyo hawakustahili kuadhibiwa. Lakini katika yote waliyopitia, bado Mitume walichagua kuhubiri Injili kwa gharama yoyote. Yaani walimchagua Mungu, na siyo Ulimwengu. Maisha unayoishi yanaakisi wewe kumchagua Mungu au Ulimwengu?

Jumatano njema

 

Heri Buberwa 

Mlutheri