Date: 
05-06-2023
Reading: 
Yohana 3:1-15

Jumatatu asubuhi tarehe 05.06.2023

Yohana 3:1-15

1 Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.

2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.

3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.

8 Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.

9 Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya?

10 Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu?

11 Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali.

12 Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni?

13 Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu.

14 Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;

15 ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.

Mungu mmoja;

Baba, Mwana na Roho Mtakatifu;

Nicodemu anamwendea Yesu usiku akimwambia kuwa ametoka kwa Mungu, na Yesu akimwambia kuwa anatakiwa kuzaliwa mara ya pili. Nicodemu Farisayo alienda usiku kwa Yesu, bila shaka hakutaka kuonekana. Lakini alimwambia Yesu kuwa yeye ni Rabii, yaani Mwalimu! Huu ni mshangao!

Yesu aliuona utupu na giza kubwa kwa Nicodemu. Ni mtu aliyemheshimu Mungu lakini bado hakuridhika, hata kumwendea Yesu usiku kwa hofu ya wenzake ili aongee na Yesu kuhusu ufalme wa Mungu. Yesu bila kuchelewa akamwambia kuwa alitakiwa kuzaliwa mara ya pili.

Nicodemu alielewa, akamwamini Yesu. Baada ya Yesu kusulibishwa, Nicodemu ndiye aliyesaidiana na Yusufu wa Armatiya kuupumzisha mwili wa Yesu kaburini. Nicodemu alitubu, aliamini, na alizaliwa tena kwa Roho Mtakatifu na kuupata uzima.

Kuzaliwa tena ni zaidi ya muonekano mpya, uwe wa kidini au vyovyote. Ni maisha mapya. Tulizaliwa dhambini lakini tumeokolewa kwa neema. Kristo anatuita kuishi kwa upya kila siku, na kutubariki ili tuupate uzima katika yeye.

Uwe na wiki njema.

 

Heri Buberwa