Event Date: 
12-04-2023

Siku ya Jumamosi tarehe 1 Aprili 2023 imefanyika ibada ya wazee katika Usharika wa Kanisa Kuu Azana Front Cathedral, jijini Dar es Salaam. Ibada kama hii huwa inafanyika baada ya kipindi maalum ili kuwapa fursa wazee ambao mara nyingi hushindwa kufika kanisani kutokana na sababu mbalimbali hususani zinazotokana na umri wao kuwa mkubwa hushindwa kufika katika ibada za kawaida kanisani hapo kutokana na kuhitaji muda mwingi wa kupumuzika majumbani mwao.

Mwaka huu 2023, ibada imewaleta wazee wa usharika pamoja na kushiriki ibada kanisani wakiwa wamesindikizwa na wasaidizi na ndugu zao wa karibu. Wazee wamepata fursa ya kubadilishana mawazo, kushiriki shughuli mbalimbali za ibada kama kushiriki chakula cha Bwana, kushiriki kuimba ritrugia pamoja na nyimbo mbalimbali.

Akizungumza katika ibada hiyo  Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt Alex Malasusa amewapongeza wazee walioweza kushiriki ibada na kuwaomba ndugu na jamaa wanaoishi na wazee hao kutosita kuwaleta kanisani wazee wao pindi fursa za ibada ya aina hiyo zinapojitokeza.

Wazee wa umri kama hawa hawasubiri mikutano ya usharika kusema wakiona jambo linaharibika, atamwita mchungaji na atamweleza. Hawa ndio wazee tunaowahitaji katika Usharika wetu,” amesema Baba Askofu.

Mwanzo 25: 8: Ndipo Abrahamu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku, naye akakusanywa pamoja na watu wake.

Akitumia mahubiri kutoka Mwanzo 25:8, Baba Askofu alisema, "Kila amtu anapaswa kutambua na kujua kuwa Mungu ana kusudi la kutupa umri huu, umri tulionao ni kusudi la Mungu. Mungu ametuacha ili tuwe na siku nyingi za kuwa karibu naye lakini kuwa baraka kwa vijana na watoto wanaotuzunguka. Hivyo basi sisi tulio wazee, tena wazee wema lazima kujua Mungu anataka jambo gani ulifanye kwa ajili ya kanisa". 

Mara baada ya ibada kumalizika wazee walipata fursa ya kukaa pamoja na kupata chai iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili yao huku wakibadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali ya kanisa na jamii kwa ujumla.

Aidha, Baba Askofu Malasusa, Msaidizi wa Askofu Dean Chediel Lwiza pamoja na Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, Mchungaji Charles Mzinga walipata nafasi ya kupita na kuwasalimu wazee katika meza zao walizokuwa wameketi wakinywa chai na kushriki huduma za kupata vipimo na matibabu vilivyokuwa vikitolewa usharikani hapo.

Kuangalia ibada hiyo: https://www.youtube.com/watch?v=ddezEylHgAI